Pata Habari Motomoto kwa kuandika E-mail yako hapo chini.


Home » , » BIASHARA YA MAMA NTILIE YATUMIKA KUSAMBAZA MADAWA YA KULEVYA JIJINI DAR

BIASHARA YA MAMA NTILIE YATUMIKA KUSAMBAZA MADAWA YA KULEVYA JIJINI DAR

 Biashara ya dawa za kulevya nchini inazidi kuchukua sura mpya ambapo sasa wanawake wanaouza vyakula, maarufu mama ntilie, hutumika kusambaza dawa hizo kwa wateja.
Uchunguzi uliofanywa kwa muda mrefu katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam unaonyesha kuwa biashara hiyo inafanyika katika maeneo ya Tandika, Manzese, Vingunguti, Temeke, Tandale, Mtongani na Keko.
Wanawake  hao wamekuwa wakitumia mwanya wa kuuza chakula kama kinga yao, huku biashara yao kubwa ikiwa ni kuuza dawa za kulevya aina ya heroin, bangi na aina nyingine.
 Mbinu hii mpya ya usambazaji wa dawa za kulevya kwa kutumia wanawake wanaouza vyakula imeelezwa kuwa inawasaidia wahusika wakuu, kuendesha biashara yao kwa ufanisi zaidi.
Uchunguzi umeonyesha kuwa wafanyabiashara wa dawa hizo wameamua kuwatumia mamalishe kutokana na kuwa waaminifu na kuhudumia wateja wengi, hivyo ni vigumu watu kuwashtukia wakiwamo askari polisi.
Imebainika kuwa dawa hizo huuzwa kulingana na maeneo, wakati maeneo ya watu wasiokuwa wa uwezo hupimwa kwa kutumia kipimo kidogo zaidi kwa bei ya chini ambayo watumiaji husika huweza kuimudu.
Aidha dawa hizo hufungwa katika mitindo miwili tofauti, ukiwa katika unga wa vidonge na wa kawaida ingawa bei zake hazitofautiani sana.
Uchunguzi unaonyesha kuwa vidoge huuzwa vikiwa vizima au vipande, huku unga wa kawaida ukiuzwa kwa kipimo maalumu.
Kwa kawaida ‘unga’ huo huuzwa kwa Sh1,000 kwa pointi huku kete moja ikiuzwa kwa Sh2,000, wakati vidonge, kizima huuzwa kwa Sh2,000, huku kipande huuzwa kwa Sh1,000 zikitofautiana kulingana na maeneo.
Gazeti hili lilifanikiwa kuongea na baadhi ya wanawake wanaojihusisha na uuzaji wa dawa hizo. 
Dada mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Asha (28) ambaye siyo jina lake halisi ni muuzaji mkubwa wa dawa hizo. Awali alikuwa akifanya shughuli zake hizo za uuzaji katika maeneo ya Yombo Kilakala, ingawaje hivi sasa amehamia Temeke.
“Unajua siku zote dhumuni la kufanya biashara ni kupata faida, hivyo naweza kusema niliingia kwenye biashara hii kwa sababu tu ina faida zaidi kuliko biashara nyingine,” anasema.
 

Copyright © 2009. MCHAMBUZI - Haki zote zimehifadhiwa