JENGO la ghorofa 19 lililojengwa karibu na Ikulu ya Dar es Salaam linadaiwa kuhatarisha maisha ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, UWAZI limefuatilia kwa umakini.
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa, jengo hilo ni refu sana na waandishi wetu waliingia humo mpaka ghorofa ya 19 kisha kuona ukaribu uliopo na kubaini kwamba ni hatari kwa usalama wa ikulu na rais mwenyewe.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili walisema kutokana na ghorofa hilo kuwa karibu na ikulu maadui wanaweza kulitumia kwa kupanda hadi juu na kuona kinachofanyika ikulu hivyo kama ni wenye nia mbaya wanaweza kutekeleza uhalifu kirahisi.
MMILIKI WAKE ANA ASILI YA NJE
Jengo hilo linalodaiwa ni la kigogo Mbongo mwenye asili ya Asia (jina tunalo) limekuwa kero katika eneo hilo kiusalama jambo ambalo limesababisha serikali kuingilia kati na kuwasaka walioruhusu ujenzi wake na kuwaburuza kortini.
Baadhi ya wakazi wa jijini Dar waliwalaumu viongozi wa serikali kwa kuacha ujenzi wa ghorofa hilo hadi kumalizika na watu kuhamia ndipo wakachukua hatua.
“Lazima tukiri kwamba kuna matatizo ya utendaji katika serikali yetu. Haiwezekani jengo linafikia ghorofa kumi na tisa ndipo serikali inaona, tunaamini walikuwa wanaona lakini waliamua kukaa kimya mpaka waliposhtuka kwamba, kumbe mtu akiwa juu anaweza kuchungulia ikulu kwa JK,” alisema mwananchi mmoja kwa sharti la kutotajwa jina.
WALINZI WA OBAMA WADAIWA KUWA CHANZO
Kuna habari kwamba, ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama nchini Tanzania Julai Mosi, mwaka huu ndiyo ulioibua mambo mengi juu ya kuwepo kwa jengo hilo kwani maafisa wake wa usalama walikataza watu kupanda hadi ghorofa ya 19 kwa maelezo kuwa wamegundua ni hatari kwa maisha ya viongozi, hasa Rais Obama aliyekuwa ikulu na JK.
Kikosi cha Majasusi wa Marekani (FBI) waliotangulia nchini miezi minne kabla ya ujio wa Obama ndiyo walioishtua serikali kwa kuwaambia watu wa usalama kuwa urefu wa jengo hilo ni hatari kwa ikulu kwa vile maadui wanaweza kulitumia.
FBI WALITEGA MITAMBO YAO JUU YA JENGO
Uchunguzi unaonesha kwamba, kwa vile FBI waliamini usalama wa ikulu ni mdogo kutokana na jengo hilo hivyo walilazimika kuweka mitambo yao juu yake na kuendelea kuwepo hapo kwa saa ishirini na nne kipindi chote cha ziara ya Obama.
FBI WALIONDOA MAGARI CHINI YA JENGO
Vyanzo vyetu vya habari ndani ya ikulu vililitonya Uwazi kuwa, mbali na FBI kuweka mitambo yao ya kiusalama, pia walilazimika kuondoa magari yote yaliyokuwa yamepaki chini ya jengo hilo na kuitahadharisha serikali ya Tanzania kuwa makini na ghorofa hilo.
WAPENDEKEZA JENGO LIVUNJWE
Habari zaidi zinasema FBI hao walipendekeza jengo hilo livunjwe ama liwe la serikali na waishi wana usalama wanaolinda viongozi wa kitaifa.
“Baada ya FBI kutoa taarifa hizo ikulu ndipo ‘mchawi’ alipoanza kutafutwa hadi kufikia hatua ya kukamatwa walioruhusu ujenzi huo,” kilisema chanzo.
KILA KITU KINAENDELEA
Waandishi wetu wamegundua kuwa pamoja na tahadhari iliyotolewa na FBI juu ya jengo hilo, lakini bado shughuli za kila siku zinaendelea sambamba na watu kuishi.
WALIOTOLEWA ‘KAFARA’ NI HAWA
Hivi karibuni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Makumba Kimweri na Msanifu Mwandamizi wa Majengo, Richard Maliyaga walipandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashitaka ya kutumia madaraka vibaya kwa kuruhusu ujenzi wa ghorofa hilo karibu na ikulu.
Washitakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo.
Washitakiwa walikana mashitaka na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini watatu wafanyakazi wa serikali waliosaini hati ya shilingi milioni 50.
Souce: Gazeti la Uwazi via Global publisher