Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania umesema hauna imani na tume iliyoundwa na jeshi la
polisi nchini humo kwa ajili ya kuchunguza tukio la kupigwa risasi kiongozi wa kidini Sheikh Ponda Issa Ponda.
Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Baruan  Muhuza Mratibu wa mtandao huo Onesmo Ole Ngurumwa amewaambia waandishi  wa habari mjini Dar es Salaam leo kuwa jeshi hilo halina haki ya  kujiundia tume ikiwa lenyewe ndiyo linatuhumiwa kumpiga risasi sheikh  huyo.
Ngurumwa amesema kuwa inasikitisha  kuona vyombo vya dola vinaendelea na uvunjaji wa sheria kwa kutumia  nguvu inayokiuka haki za msingi za binadamu.
Msemaji wa Jeshi la polisi nchini  humo Advera Senso ameiambia BBC mjini Dar es Salaam kuwa jeshi lake kwa  kushirikiana na jukwaa la haki jinai wameunda kikosi kazi kwa ajili ya  kufanya uchunguzi wa tukio hilo huku akikana kuwa Sheikh Ponda alipigwa  risasi na polisi.
Senso amewalaumu wafuasi wa Sheikh  Ponda kwa kuwazuia askari kumkamata Sheikh huyo kwa kuwarushia mawe,  hatua iliyosababisha askari hao kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya  na hata hivyo wafuasi hao walifanikiwa kumtorosha kiongozi huyo wa  kidini.
Mapema Jumatatu asubuhi Baraza la  waisilamu Tanzania-BAKWATA limeunga mkono kauli ya Jumuiya ya taasisi za  kisilamu na kuitaka serikali kuchunguza kwa kina tukio lililosababisha  kupigwa risasi kwa Katibu huyo wa Shura ya Maimamu nchini humo.
Kaimu Sheikh Mkuu wa Tanzania Alhad  Mussa Salum amezungumza na waandishi wa habari Mjini Dar es Salaam na  kusema kuwa japokuwa BAKWATA imekuwa ikipingana na misimamo ya Sheikh  Ponda limesema serikali ilikuwa na nafasi ya kumkamata Ponda kwa kufuata  mkondo wa sheria.
Sheikh Ponda amekuwa katika mivutano  ya mara kwa mara na serikali ya Tanzania, anadaiwa kupigwa risasi baada  ya kutokea vurugu kwenye mkutano wa mawaidha ya baraza la sikukuu ya Idd  el Fitr Jumamosi jioni.
Awali siku ya Jumapili Mwenyekiti wa  Shura ya Maimamu Tanzania, Alhajj Mussa Kundecha, aliwaambia waandishi  wa habari mjini Dar es Salaam kuwa endapo serikali haitachukua hatua  itakayowaridhisha Waislamu, wataamua kufikiria upya mustakabali wao na  serikali ya nchi hiyo.
Sheikh Ponda amelazwa katika  hospitali ya Taifa, Muhimbili, mjini Dar es Salaam akiuguza jeraha la  risasi huku akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu.
Taarifa za jumuiya hiyo ambayo  inajulikana zaidi Tanzania kama Shura ya Maimamu zinasema kuwa Sheikh  Ponda ambaye polisi wanasema walikuwa wakimtafuta kwa tuhuma za kutoa  matamko ya uchochezi, alisafirishwa usiku kutoka mji wa Morogoro hadi  Dar es Salaam zaidi ya kilomita 200.
Sheikh Ponda kwa sasa anatumikia  kifungo cha nje cha mwaka mmoja alichohukumiwa mapema mwaka huu baada ya  kukutwa na makosa kadhaa ikiwemo uchochezi wa kuharibu mali za watu.
BBCswahili.
