“Ninatoa dakika 10 kwa aliyeingia na mavazi ambayo hayatakiwi kanisani humu kutoka mara moja akavae vizuri, la sivyo ndoa yao haitafungwa,” alisema Padri Haule wa Kanisa hilo lililoko Oysterbay, Dar es Salaam.
Awali vurugu hizo zilizotokea Jumamosi iliyopita, zilianzia nje, wakati Katekista wa Parokia hiyo, Yohane Maboko, alipotangazia wanandoa na ndugu zao waliokuwa mabega wazi au kuvaa nguo fupi, kutafuta nguo za kujifunika au wasiingie kabisa kanisani.
Maharusi walikubali kutekeleza ombi hilo, wakavishwa vitambaa mabegani vya rangi tofauti na gauni jeupe la harusi, wakaruhusiwa kuingia kanisani, tayari kufunga pingu zao za maisha.
Hata hivyo, mmoja wa ndugu wa maharusi hao ambaye jina lake halikupatikana mara moja, alipotaka kulazimisha kuingia na kivazi chake cha mabega wazi, alizuiwa na Katekista Maboko. Katekista huyo alimfuata mwanamke huyo ili kumrudisha akavae vizuri, lakini aliibua zogo na kulazimisha kuingia na vazi hilo.
Zogo hilo lilipoendelea, wanandugu waliingilia kati, wakitetea vazi hilo ambapo mmoja wa wanandugu, alimvua miwani Katekista Maboko na kuipiga chini ikavunjika huku yeye na wenzake wakimtolea maneno makali ya kumtaka asimzuie ndugu yao kuingia kanisani.
Wakati ndugu hao wakimdhibiti Katekista Maboko, mwanamke huyo alitumia mwanya huo na kupenya hadi ndani ya Kanisa, ambamo Padri Haule, alikuwa akijiandaa kuanza ibada.
Baada ya Padri Haule kupata taarifa, alitangaza kuwa ndoa ya maharusi wa msichana huyo, haitafungwa hadi awe ametoka.
Licha ya Paroko kutangaza hivyo, bado ukaidi uliendelea jambo lililomfanya Katekista Maboko kumfuata tena dada huyo na kumwamuru atoke nje, ambapo aliendelea kupinga na baadaye akatekeleza amri hiyo ya Paroko.
Baada ya hapo shughuli za kufungisha ndoa ziliendelea kwa amani na utulivu hadi mwisho maharusi wakatoka kwenda kuendelea na mambo mengine.
Akizungumza na mwandishi wetu, Katekista Maboko alisema waumini hao walikiuka maadili ambayo Kanisa lina wajibu wa kulinda na kuyasimamia ili waumini wake wayafuate.
Alisema miwani yake iliyovunjwa ilikuwa na thamani ya Sh 90,000 na baada ya ibada hiyo, aliyetenda kosa hilo alimwendea na kumwomba radhi na kulipa Sh 50,000 na kuahidi kumalizia kiasi kilichobaki wakati wowote.
Maboko alisema uvaaji wa mavazi yasiyotakiwa kanisani hapo, umekuwa ukipigiwa kelele mara kwa mara, na hata katika mafundisho ya ndoa huambiwa lakini ukaidi unaendelea. “Maharusi wakati wa mafundisho ya ndoa tunawaambia kuhusu mavazi yao na hata ya ndugu zao watakaowasindikiza kanisani, kuwa wavae kistaarabu lakini hawasikii,” alisema Katekista Maboko.
Makanisa mengi siku hizi yamekuwa yakipiga marufuku uvaaji wa nguo fupi na zinazoacha mabega wazi kwa wasichana na wanawake, wakati wa ibada za kawaida na za ndoa.