UTATA mkubwa umezidi kugubika tukio la kulipuka kwa bomu katika mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika mwishoni mwa wiki na kujeruhi mtu mmoja, baada ya Jeshi la Polisi na mbunge huyo kila mmoja kutishia kuchukua hatua za kisheria.
Wakati Jeshi la Polisi likikanusha kulipua bomu hilo kwa nia ya kumuua mbunge huyo, CHADEMA imesema imelishitaki jeshi hilo Mkoa wa Kinondoni kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa madai ya kulipua bomu kwa kusudi la kudhuru maisha ya mbunge wake.
Kaimu Katibu wa chama hicho Jimbo la Ubungo, Ali Makwilo akiongea na waandishi wa habari jana, alisema polisi walilipua bomu katika eneo alilokuwepo Mnyika akifanya mazungumzo na askari hao.
“CHADEMA tunaamini kwamba haki za binadamu watashughulikia mashtaka hayo kwa kuzingatia mamlaka na majukumu iliyopewa na katiba na sheria za nchi ya kupokea malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu na kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki hizo,” alisema.
Hata hivyo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imesisitiza kwamba bomu hilo halikulengwa kwa Mnyika na kukanusha kujeruhiwa kwa mtu kama inavyovumishwa.
Naibu Kamishna wa Kanda hiyo, Ally Mlege aliwaambia waandishi wa habari kuwa CHADEMA ilikuwa ifanye mkutano wa hadhara Julai 21 mwaka huu katika Uwanja wa Sahara uliopo Mabibo na kuhutubiwa na Mnyika kinyume cha taratibu.
Mlege alisema hakuna bomu lililorushwa, isipokuwa askari namba E.5340 D/CPL Julius aliyekuwa ndani ya gari ya polisi lenye namba za usajili PT 1902 alikuwa akisogeza sanduku la mabomu ya machozi ya kurusha kwa mkono na bahati mbaya moja likalipuka.
“Mnyika alikubaliana nasi na kuwatangazia wafuasi wake kuwa mkutano eneo lile umezuiliwa hivyo waelekee Ubungo ambako walikuwa na kibali kutoka polisi wa Kimara nao waliondoka eneo hilo bila madhara yoyote,” alisema Mlege.
Alidai kusikitishwa na habari za uzushi kwamba bomu hilo lilimkosa mbunge huyo na kuwataka waandishi wa habari kuacha kupotosha umma ukweli wa suala hilo na kutishia kwamba jeshi hilo litawashughulikia.
Mbali na bomu hilo, chama hicho kimelaani hatua ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Saalam kusitisha mkutano wa hadhara ulioandaliwa katika Uwanja wa Sahara kwenye Kata ya Mabibo uliopangwa Julai 21.
Alisema polisi walidai sababu za uwepo wa ziara ya Makamu wa Rais, Dk. Gharib Billal katika Wilaya ya Kinondoni zilikuwa ni za uongo kwa kuwa kiongozi huyo hakuwa na ziara katika Jimbo la Ubungo siku hiyo.
“Kutokana na hali hiyo tunalitaka Jeshi la Polisi kueleza kwa chama na kwa wananchi sababu halisi za kuzuia mkutano huo na kufahamu kuwa ni nani katika Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam aliyetoa maelekezo ya mkutano huo kusitishwa,” alieleza Makwilo.
Alisisitiza kuwa chama hicho kilifuata taratibu zote za kuwasilisha taarifa kwa Jeshi la Polisi kupitia barua yake ya tarehe 17 Julai kwa Kanda Maalumu Dar es Salaam ambayo nakala iliwasilishwa ofisi ya Polisi Mkoa wa Kinondoni na Polisi Wilaya ya Magomeni kama utaratibu uliowekwa na jeshi lenyewe.
Makwilo alieleza kuwa wamechukua ushahidi wa jumla ya magari matatu ya polisi yaliyokuwa katika eneo la uwanja yakiwa na askari na silaha na mengine zaidi yalikuwa yameandaliwa katika eneo la jirani kwa ajili ya kuongeza nguvu kama kungezuka vurugu.
Mnyika afafanua
Akifafanua ukweli wa kile kilichotokea, Mnyika alisema maelezo ya polisi sio ya kweli, na hawezi kuacha kuamini kuwa bomu hilo lililengwa kwake.
“Bomu lililipuka wakati niko katika dirisha la gari la polisi. Sio kweli nilikuwa pembeni nazungumza na wananchi na eti tuliondoka salama.
“Na kwa sababu ametoa maelezo ya uongo, lazima sasa waseme ukweli wa siri hiyo. Kwanini mabomu yalipuke tu kwenye mikutano wa CHADEMA, na sio CCM?” aliuliza Mnyika.
Mbunge huyo pia alisema sababu za polisi kuzuia mkutano wake hazina ukweli wowote, kwa kuwa kama kweli hawakuwa na askari wa kutosha kulinda mkutano wake, ilikuwaje wapatikane wa kujaza gari tatu na silaha kwa ajili ya kumdhibiti.