Imeelezwa kuwa, uhaba wa maji katika Chuo cha Ualimu Murutunguru wilayani Ukerewe, umesababisha athari kadhaa kwa wanachuo, ikiwa ni pamoja na matukio ya ujauzito kwa wanachuo wa kike.
Hayo yalibainika hivi karibuni wakati wa mahafali ya 19 kwa wahitimu wa mafunzo ya ualimu daraja la III A yaliyofanyika chuoni hapo.
Katika risala ya Mkuu wa Chuo hicho kilichoanzishwa miaka 61 iliyopita, Augustine Sahili alisema miongoni mwa wanachuo 14 wa kike waliopaswa kuhitimu mwaka huu, sita walikatisha masomo kutokana na ujauzito.
Alifafanua kuwa, wanachuo hutumia muda mwingi kutafuta maji nje ya chuo, hivyo kujikuta wakiingiza katika majaribu ya kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na matokeo yake ni baadhi ya wanachuo wa kike kuishia kupata ujauzito.
Alisisitiza pia kwamba, mbali ya adha wanazopata wanafunzi wa kike, kero ya maji kwa ujumla imekuwa ikichangia kuwavurugia wanachuo utaratibu wa kufuata ratiba za masomo.
Mkuu huyo wa chuo alisema tatizo hilo limedumu kwa miaka mingi, kwani wakati chuo kinaanzishwa mwaka 1952, kulikuwa na kisima kimoja chenye uwezo wa kuhudumia watu 70 lakini idadi ya watu kwa sasa imefikia 555, lakini havijapatikana vyanzo vingine vya maji.
Wakati mkuu wa chuo akiyasema hayo, wanachuo kwa upande wao, kupitia risala iliyosomwa na Joel Biganza wameshauri kuimarishwa kwa miundombinu ya chuo huku wakiitaka Serikali kuangalia upya ufaulu kwa mwalimu kupimwa kwa somo moja la utambuzi wa ualimu linalohusisha saikolojia, tathmini, maandalio na uchunguzi.
Akizungumzia somo hilo, mkuu wa chuo, Sahili alisema anayefanya vibaya katika somo hilo anakuwa ameshindwa na kuongeza kuwa mwaka jana wahitimu watatu walishindwa na kurudishwa nyumbani.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Maiga Joseph aliutaka uongozi wa chuo hicho kufikisha kilio cha maji kwa mamlaka husika ili iangalie jinsi ya kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
Katika mahafali hayo, walimu 330 walihitimu na kupata cheti cha ualimu daraja la III A, idadi ambayo inatarajiwa kuendelea kupunguza kero ya upungufu wa walimu nchini.