JESHI la Polisi Kituo cha Pangani, Ilala Dar es Salaam limemnasa kijana mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Abdallah kwa tuhuma za kuwawekea wanawake madawa ya kulevya katika vinywaji kisha kuwaibia
Ishu hiyo ilijiri Jumatatu iliyopita katika baa moja iliyopo Amana, Ilala jijini Dar es Salaam ambapo baada ya kunaswa, mlalamikiwa huyo alipelekwa katika kituo hicho cha polisi kwa hatua zaidi.Kwa mujibu wa chanzo chetu, mtuhumiwa alitiwa mbaroni baada ya kuwekewa mtego uliomnasa.
“Polisi walikuwa wakimsaka kwa muda mrefu kutokana na madai ya kuwatilia ‘unga’ watu, hasa wanawake kwenye vinywaji kisha kuwaibia.
Huyu ndiye mtuhumiwa wa kuwawekea wanawake madawa ya kulevya katika vinywaji kisha kuwaibia aitwaye Abdallah.
“Nasikia ameshawaliza wanawake wengi wakiwemo vigogo,” kilisema chanzo hicho.Siku ya tukio, Abdallah alikuwa kwenye baa hiyo bila kujua kuwa polisi walikuwa wakimuwinda, ndipo walimpomzingira na kumnasa.
Inaelezwa kuwa baada ya habari hii kutoka, wanawake wengi watamiminika kituoni hapo kutoa malalamiko yao juu yake.
Mwandishi aliingia Kituo cha Polisi Pangani na kumuuliza afande mmoja kuhusu sakata la kijana huyo, alikiri lakini akasema yeye si msemaji wa polisi.
“Ni kweli tunamshikilia Abdallah kwa tuhuma za kuwalewesha watu, hasa wanawake, kisha kuwaibia vitu vyao kama vile simu, fedha, mikufu ya dhahabu, hata kuwavua viatu. Huyafanya hayo gesti au baa lakini siwezi kukueleza kwa undani kwani mimi si msemaji wa polisi,” alisema askari huyo.