Mojawapo ya ofisi za Kampuni ya Kanumba The Great Films illiyopo Sinza Mori.MIPANGO endelevu inapaswa kufuatwa na kila mwanadamu, katika familia zetu za Kiafrika mara nyingi tunaanguka katika suala la mipango mikakati ya muda mrefu. Mwanadamu akifariki, mara nyingi wanaoachwa kuendeleza kazi za marehemu wanaishia kusuasua na kutofikia malengo.Yapata mwaka mmoja tangu, aliyekuwa legend wa simema za Kibongo, Steven Kanumba ‘The Great’ afariki dunia na kuiacha Kampuni yake ya Kanumba The Great Film ikiendeleza shughuli zake za kuzalisha filamu kama kawaida.
Kampuni aliyoiacha pale Sinza-Mori, jijini Dar ilibaki chini ya mikono ya wafanyakazi wake wakiongozwa na mdogo wa marehemu, Seth Bosco, mpiga picha za video, Zakayo Magulu pamoja na Mayasa Mrisho ‘Maya’ ambaye alikuwa akifanya kazi kama msimamizi wa ‘location’ (location manager) na masuala ya makeup.
Kadiri siku zilivyozidi kusonga, umoja kati yao ulianza kupungua. Kila mmoja anaonekana kuhangaika kivyake licha ya kwamba kampuni bado ipo. Mikakati ya jumla ikawa haijadiliwi, kila mmoja akawa anaangalia namna ya kujikwamua kivyake.
Mara kadhaa nimekuwa nikizungumza na baadhi ya wasanii waliokuwa tegemezi katika kampuni hiyo, wamekuwa wakiniambia wapo bize kufanya kazi zao binafsi nje ya Kanumba The Great Film. Hiyo inaonesha dalili kwamba kazi za umoja zimeanza kulegalega.
Miongoni mwa bidhaa zilizokuwepo katika ofisi hiyo ni pamoja na DVD za marehemu alizokuwa akiziuza lakini baada ya kifo chake, ofisi hiyo imepoteza mvuto wa kibiashara na hata mpangilio kwa jumla. Hakuna mtu wa kukemea au kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.
Kabla Kanumba hajapatwa na mauti, alikuwa mpiganaji. Alipambana kuhakikisha anafikia malengo yake. Lengo lake lilikuwa ni kuhakikisha tasnia ya filamu inafika levo za Kimataifa.
Enzi za uhai wake, Kanumba ndiye aliyeanza kuthubutu kutoboa mianya ya kuwashirikisha wasanii wa Nigeria. Alifanikiwa kucheza simema ya Dar 2 Lagos na filamu nyingine kadhaa kwa kuwashirikisha wasanii mbalimbali wa nje ya Tanzania.
Kama hiyo haitoshi, mwaka 2011 marehemu alizidi kujitanua zaidi katika soko la Nollywood kwa kumchukua mwigizaji mkubwa nchini Nigeria, Ramsey Noah na kufanya naye filamu ya Devil King Dom ambayo kwa kiasi kikubwa imeleta mapinduzi makubwa katika gemu.
Kuonesha anapenda maendeleo, Kanumba hakuishia hapo kwani mwaka huohuo alipiga hatua nyingine kubwa katika sanaa baada ya kufanikiwa kwenda New York, Marekani na kununua vifaa vya kisasa vya kuzalishia filamu.
Mpaka mauti yanamkuta Aprili 7, mwaka jana tayari alikuwa ameshajiwekea misingi mizuri katika sanaa kwani alikuwa anamiliki kampuni yenye vifaa vya kisasa pamoja na kutoa ajira ya wafanyakazi wasiopungua kumi.
Marehemu alijiwekea mikataba na Kampuni ya Steps Entertainment kuzalisha filamu 6 kwa mwaka. Hilo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa, tena aliweza kuigiza na filamu nyingine za kushirikishwa mbali na zile za Steps.
Hadi kufikia Aprili 7, mwaka huu marehemu alikuwa akitimiza mwaka mmoja kaburini. Mdogo wake, Seth Bosco ambaye amejitoa kuendeleza kampuni hiyo, amefanikiwa kuingiza sokoni filamu tatu tu.
Mbaya zaidi mbili kati ya hizo (Love and Power na Ndoa Yangu) zilisharekodiwa na marehemu, wao wakazikamilisha kwa kuzifanyia ‘editing’. Yeye kama yeye alifanikiwa kuingiza filamu moja sokoni ya Malaika.
Kwa mwendo huo utagundua spidi aliyoiacha marehemu imepungua, filamu walizoingiza ni chache sana. Kifupi wanasuasua kama si kupoteza muelekeo. Kwa mfumo aliokuwa akienda nao marehemu, mwaka mmoja baada ya kifo hadi sasa, kampuni ilipaswa kuzalisha filamu sita au zaidi.
Kuna kitu cha kujifunza katika mfumo ambao aliuacha marehemu. Walioachiwa kampuni wakiongozwa na Seth wanapaswa kujitazama upya.
Hii ni changamoto ngumu inayohitaji akili ya ziada kuweza kuvuka, katika hali kama hiyo hakuhitaji masihara wala utani hata kidogo. Hapo ndipo watu wanapotafutana uchawi. Wenye mamlaka ya kuiendesha kampuni kwa namna moja au nyingine wanapaswa kuwa wakali kidogo ili mambo yaende.
Kujituma kwa marehemu ndiyo kulisababisha ashinde tuzo mbalimbali za filamu zikiwemo zile za Zanzibar Film Festival (Ziff). Ingependeza basi heshima ile aliyoiacha marehemu ikaenziwa kwa kuvuka mipaka, ikiwezekana zaidi ya pale alipokuwa akipapigia mahesabu yeye enzi za uhai wake.
Naamini inawezekana kama wahusika wataweka nia.
Home
»
skendo mastaa
»
BAADA YA MWAKA MMOJA TANGU KIFO CHA KANUMBA-'KAMPUNI YA KANUMBA THE GREAT YAPUMULIA MASHINE'