Pata Habari Motomoto kwa kuandika E-mail yako hapo chini.


Home » » USICHOKIFAHAMU KUHUSU ASILI NA AINA YA WACHAGA

USICHOKIFAHAMU KUHUSU ASILI NA AINA YA WACHAGA


Kabila la Wachaga linafahamika kwa wengi kuwa linapatikana mkoani Kilimanjaro.Kwa asili, Wachaga ni mchanganyiko wa Wamasai, Wasambaa, Wataita, Wakamba na Wakahe.
Wachaga walianza kuhamia kwenye miteremko ya Mlima  Kilimanjaro kwenye karne ya 17.
Walipofika wakiwa katika vikundi vidogovidogo waliwakuta wakazi, wenyeji kwenye Misitu ya Mlima Kilimanjaro walioitwa ìWakonyingo..
Wenyeji hawa ambao huitwa Mbilikimo hawakupenda kuchanganyika na wahamiaji wageni, hivyo wakahama na kuanzisha makao yao ya kudumu kwenye misitu minene iliyopo nchini Kongo.
Watu wengi wanafikiria kwamba Wachaga wanatokana na asili moja. Ukweli ni kwamba  wamegawanyika katika himaya 15, wanatofautiana kwa lafudhi, lugha, rangi na mwonekano wa miili yao.Wachaga wapo katika makundi makuu matatu ya Hai, Vunjo na Rombo.
Wale wanaopatikana eneo la Hai ni Wasiha, Wamasama, Wamachame,Wangíuni, Wakibosho, Wauru na Wamoshi. Kwa wale wanaopatikana eneo la Vunjo ni Wakirua, Wakilema, Wamarangu, Wamamba na Wamwika.
Kutoka eneo la Rombo ni Wamkuu, Wamashati na Wasseri.
Hadi sasa haijulikani vizuri asili ya jina Wachaga, ila wanahistoria wanaeleza kwamba jina  hilo linatokana na neno la Kiswahili linaloitwa 'Kichaka'.
Inaelezwa kwamba misafara ya wafanyabiashara iliyokuwa ikiongozwa na Waswahili pamoja na Waarabu, walipokuwa wakipita maeneo ya Vunjo waliwaona wenyeji wa huko wakiwa wamejenga vibanda vya kulinda mazao yao yasiliwe na wanyama waharibifu.
Wakawaita wenyeji hawa kwamba wanaishi vichakani na kuanzia hapo wageni wafanyabiashara na Wamisionari walipokuwa wanakuja Kilimanjaro walielekezwa na waongozaji misafara yao kwamba wanakwenda kwenye nchi ya ìUchakani,î, wakimaanisha kwamba kwa watu wanaoishi vichakani.
Hatimaye wageni wakashindwa kulitamka vizuri neno hili na kuliita ìUchagani,
Jina hili likawekwa kwenye ramani na kuitwa nchi ya ìWachaga.î Hivyo ndivyo wenyeji waliokuwa wakiishi kwenye Miteremko ya Mlima Kilimanjaro walivyopewa jina lao. Wachaga.
Maendeleo ya Wachaga
Maendeleo yao hapo awali yalitokana na zao la kahawa. Walifanikiwa kuanzisha vyama vya ushirika na hatimaye   mwaka 1932 walianzisha Halmashauri ya Wachaga (Chaga Council) ambayo kwa sasa inatumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi.
Halmashauri hii iliongozwa na Mangi Mkuu ìMshumbue Thomas  Marealle II.
Mwaka 1946, utawala wa Waingereza uliboresha Baraza la Halmashauri ya Wachaga. Himaya ndogo za Wachaga zipatazo 17 (himaya mbili za  Wakahe na Waarusha chini zilijumuishwa kwenye Tarafa ya Vunjo) na kuundwa kwa Tarafa tatu za Hai, Vunjo na Rombo.
Halmashauri ya Wachaga ilijenga miundombinu  na huduma za jamii ikiwamo kuwasomesha watoto wao kwenye shule na vyuo mbalimbali  kama Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda.
Halmashauri ya Uchaga ilikuwa na bendera yake  ambayo ipo hadi leo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, yenye nembo tano kuu:
1- Mlima Kilimanjaro uliochorwa katikati ya bendera ukionyesha mandhari nzuri ya kilele cha Kibo. Kilele cha Kibo kinatoa maji safi na ni kielelezo cha umoja wao.
2- Chini ya kilele cha Kibo, upande wa kushoto wa bendera kuna mgomba wenye ndizi. Hiki ni chakula kikuu cha Wachaga.
3-  Upande wa kulia wa bendera ni tawi la mbuni ukiwa na matunda yake. Kahawa ni zao lililowaletea  maendeleo.
4-   Bendera imezungukwa na  matawi ya 'sale' lenye matawi mawili (draceana plant). Matawi  haya yamefanya mduara kuzunguka kilele cha Kibo, mgomba wa ndizi na tawi la zao la kahawa. Masale ni mmea unaoheshimiwa sana na Wachaga wote.
Ni alama ya amani. Masale hutumika katika sherehe na shughuli zote za kimila zinazofanywa na Wachaga. Majani yake ni kijani kibichi yanayoonyesha jinsi Kilimanjaro ilivyo na rutuba nzuri inayostawisha mazao ya kila aina.
5-    Juu kidogo ya kilele cha Kibo yupo chui ambaye amejipumzisha. Chui ni alama kuu ya mamlaka ya Wachaga.
Hapo awali kwenye miteremko ya Mlima Kilimanjaro walikuwepo chui wengi wa rangi nyeusi lakini kutokana na ongezeko la watu pamoja na uharibifu wa mazingira chui hawa wametoweka.
Sikukuu ya Wachaga
 Sikukuu ya Wachaga wote ilikuwa ikiadhimishwa Novemba 10  kila mwaka kama kumbukumbu ya siku ambayo Wachaga wote walipokusanyika na kumchagua Mangi Mkuu  baada ya kuteuliwa na Halmashauri Kuu ya Uchaga.
Maadhimisho ya kwanza ya mwaka 1952 yalitanguliwa na uchaguzi wa Halmashauri ya Wachaga wote kuanzia kwenye ngazi ya Uchili (kijiji), Umangi ( uchifu wa eneo) na mwisho ngazi ya baraza kuu.
Sherehe ziliadhimishwa mjini Moshi ambako Wachaga wote pamoja na wageni waalikwa kutoka mataifa mbalimbali walikusanyika katika Viwanja vya Halmashauri ya Uchaga (sasa ni makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, [Kilimanjaro District Council-KDC]) kushuhudia sherehe kubwa na yenye kusisimua sana.
Jumba la Makumbusho
Upo umuhimu mkubwa wa kuhifadhi historia ya Wachaga kama kumbukumbu sahihi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Pia, ipo haja kwa majengo ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi pamoja na Ikulu yakarejeshwa kwa Wachaga ili yageuzwe kuwa majengo ya kuhifadhi kumbukumbu  ya kabila  hilo.
Katika majengo haya patahifadhiwa nyaraka zote za Chaga Council ambazo baadhi zimeshaanza kutoweka, kutahifadhiwa pia shughuli za mila na kiutamaduni tangu enzi ya karne ya 18.
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi haina budi kutafuta eneo  la kujenga  majengo mapya badala ya kuyatumia ya kihistoria.
 

Copyright © 2009. MCHAMBUZI - Haki zote zimehifadhiwa