Pata Habari Motomoto kwa kuandika E-mail yako hapo chini.


Home » » FAHAMU NAMNA YA KUJIPANDISHA THAMANI KWA MPENZI WAKO

FAHAMU NAMNA YA KUJIPANDISHA THAMANI KWA MPENZI WAKO

Nazungumzia kuhusu thamani. Ni somo linalohitaji utulivu mkubwa wa akili na utayari wa ubongo. Ninaposema kushuka thamani namaanisha kupungua kwa umuhimu au kupotea kabisa.
Kubwa ambalo utakuwa umebaki nalo (labda) ni kukutana kwa ajili ya mapenzi tu. Hawezi kukushirikisha katika mambo yake kwa sababu huna thamani kwake.
Kwa bahati mbaya ni kwamba, ukishushwa thamani, mara nyingi unaweza usigundue hilo hivyo kuendelea na maisha kama kawaida katika mtindo ambao kumbe tayari mwenzako ameshakubadilisha daraja.  
UTAJUAJE KUWA UMESHUSHWA THAMANI?
Ninachohitaji kuzungumza nanyi marafiki zangu ni namna ya kujipandisha thamani ili mpenzi wako asikuchoke wala kukushusha au kukuona wa kawaida. Kila wakati akione wewe ni muhimu na akufanye namba moja katika maisha yake lakini kabla sijafika hapo nataka kwanza mfahamu dalili atakazozionyesha mwenzako kuonesha kwamba ameshakushusha thamani.
(i)  Mawasiliano hupungua
Hapa inategemea na kasi ya mawasiliano mliyokuwa nayo mwanzoni lakini kwa kiwango chochote kile huanza kupungua. Kama alikuwa na kawaida ya kuwasiliana nawe mara kwa mara akikueleza mambo mbalimbali – hata madogo tu, kuhusu mwenendo wa siku yake, ataacha.
(ii) Msiri kupitiliza
Kulingana na kiwango cha uhusiano wenu, ataanza kuwa msiri kwa baadhi ya mambo yake. Hata kama anafanya jambo fulani zuri kwa ajili ya maisha yenu ya baadaye, hatakuambia. Unaweza kushtukia tu kusikia kwa watu kuwa mwenzako ameagiza gari au amenunua kiwanja mahali  na pengine ameshaanza ujenzi bila kukujulisha.
(iii) Hukupuuza
Kama awali alikuwa na kawaida ya kukusikiliza, sasa ataanza kukupuuza. Unaweza kumwambia jambo lenye manufaa makubwa sana kwenu lakini asilichukulie umakini. Hii ni dalili kwamba wewe huna thamani kwake.
(iv) Hataki maswali
Mara nyingi mtu wa aina hii huwa na tabia ya kutokutaka kujadiliana kwa hoja. Kwa mfano hataki kuulizwa alipokuwa na ratiba zake zijazo. Huanza kuwa na jazba na hataki kabisa maswali yoyote kuhusu utaratibu wa maisha yake.
SIFA ZAIDI...
Kama umeshushwa thamani unakuwa kwenye hatari ya kuachwa. Hata kama mwenzako alikuwa ameshafikiria suala la kuingia kwenye ndoa na wewe lakini kwa sababu ameshakushusha thamani ndoa inaweza kuyeyuka.
Ukiwa kwenye ndoa ni hatari zaidi maana mwenzako hukuchukulia wa kawaida – mazoea huzidi na hapo ndipo uhitaji wa kuwa na mwingine wa pembeni unapoanzia. Haoni cha muhimu tena kwako, ndiyo maana wazo hilo huvamia ubongo wake kwa kasi sana.
Itafikia hatua, kama upo ndani ya ndoa, mwenzako atagoma kuongozana na wewe na kama ikitokea hivyo mkikutana na rafiki zake njiani hatakutambulisha. Hisia kwamba hamuendani humwingia.
UNAFANYAJE SASA?
Kubwa unalotakiwa kufahamu rafiki yangu mpendwa, suala la kupanda au kushuka thamani lipo mikononi mwako. Yapo mambo ambayo ukiyazingatia, mwenzako hawezi kukuchoka na kufikia hatua ya kukushusha thamani.
Tayari tumeshaona athari zake lakini hapa sasa nataka kukupa mbinu ambazo ukiwa nazo makini basi itakuwa rahisi kwako kubaki namba moja na mtu muhimu zaidi (ndiyo inavyotakiwa kuwa) kwa mpenzi wako maana ni haki yako.
ANZIA MWANZO
Ni rahisi zaidi kulinda thamani yako kuanzia mwanzo wa uhusiano wenu. Ikiwa tayari mmeshakomaa halafu tatizo hilo likajitokeza, hutumika nguvu nyingi zaidi kulirekebisha kuliko kujizatiti kuanzia mwanzo wa uhusiano. Ni mambo gani hayo? Twende hapo chini.
CHUNGA KAULI ZAKO
Naomba ieleweke wazi kuwa mada hii ni maalum zaidi kwa wanawake. Kitu muhimu cha kwanza kabisa kwa mwanamke ambaye anataka kuilinda thamani yake kwa mpenziwe ni kupima sana kauli zake.
Acha kuropoka hovyo, pima maneno yako na ikiwezekana kama unadhani kuna jambo huna uhakika nalo usizungumze kabisa. Katika eneo hili, uwe makini zaidi mnapokuwa na watu wengine. Kama mwanamke usiwe mchangiaji hoja sana.
Utulivu wako unaweza kuwa silaha kubwa ya kukufanya ubaki na thamani yako kama mwanamke anayejitambua.

 

































USIRUHUSU MAPENZI
Msichana mwenye kujitambua na kufahamu thamani yake sawasawa hawezi kuruhusu mwili wake ujulikane na mwanaume harakaharaka. Onesha unajitambua na usikubali kirahisi kuuacha mwili wako uchezewe.
Mpe hoja; kwanza mapema, hajakuoa wala kukuchumbia, haraka ya nini? Wakati unawaza kuhusu kutoa penzi lako, lazima ufikirie kuhusu athari zinazoweza kukupata kwa kukurupukia mapenzi. Mwanaume ambaye bado hamjachunguzana na huna uhakika naye wa kutengeneza maisha, kichwani mwake hakuweki kwa asilimia kubwa.
UMEJIFUNZA KITU?
Wepesi wa kutoa penzi na kujiachia na mwanaume ambaye hajakuoa huhatarisha nia ya ndoa. Ikumbukwe kwamba, si kila mwanaume anafaa kuwa mume na si kila mwanamke ni mke. Utajuaje uliyekutana naye kama ndiye au siye? Ni fumbo.
Wengine wanahamia kabisa kwa wanaume au wanakwenda weekend kufua na kufanya usafi wa nyumba. Ni makosa makubwa. Unadhani ataharakishia ndoa ya nini wakati kila kitu anapata? Amka dada yangu, tupo kwenye dunia nyingine.
SIKIA HUU USHAHIDI
Kijana mmoja ambaye hapa nitamtaja kwa jina moja la Jully, alinifuata kunitaka ushauri. Yeye anasema amejikuta amepoteza msisimko kwa mpenzi wake aliyedumu naye kwa miaka minne na anataka kumuacha ili aoane na mwingine.
Jully anasema: “Sikufichi kaka Shaluwa, nilimpenda sana Sarafina lakini sasa nahisi kama sikuwa sahihi kuwa naye. Kwanza ni mwepesi...hakunisumbua sana wakati namfuatilia, mbaya zaidi ameshatoa mimba zangu nne, wanini mwanamke kama huyo?”
Nilipomwuliza kuhusu mwanamke anayetaka kumuoa alisema: “Huyu anaitwa Veronica, nilikuwa naye kabla ya Sarafina. Wakati huo alikuwa sekondari, amemaliza UD mwaka jana (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam). Ana msimamo hatari! Mpaka ninavyozungumza na wewe hajawahi kunipa penzi na mpaka sasa amenithibitishia kwamba bado ana usichana wake. Kwa nini nisimuoe mwanamke huyu mzuri, anayejitambua na kujitunza? Hawezi kunisumbua kwenye ndoa yangu kama Sarafina.”
WANAWAKE MPO?
Kwahiyo mmeona kumbe wanaume japo wanawalaghai muwape penzi haohao ni hodari wa kuwasema vibaya na kuwashusha thamani wakati wakiwaza kuhusu ndoa. Ni vizuri wanawake mkaamka na kujitambua na kufahamu thamani mliyonayo.
Acha kudanganyika, penzi si kigezo cha upendo wa dhati. Mbona mambo yako wazi tu! Kama anakupenda atume wazee nyumbani kwenu, taratibu muhimu zifanyike, uolewe kwa heshima na thamani yako ikiendelea kuwa juu. Mwanaume wa aina hiyo ni vigumu kukutesa.
ATHARI ZA KUHARAKISHA FARAGHA
Wiki iliyopita nilifafanua zaidi matatizo ya moja kwa moja ambayo mtu anaweza kuyapata kwa kuharakisha faragha ambapo nilisema kwamba kuna suala la kuchokwa na kuonekana wa kawaida.
Lingine ni kuonekana mwepesi kwenye suala la mapenzi hivyo mwanaume kuwa na mashaka kwamba hata kama akifikia uamuzi wa kukuoa unaweza kuwa mwepesi kutoa penzi kwa wengine kama ulivyofanya kwake. Tuangalie vipengele vinavyofuata.

(i) Hupunguza thamani
Heshima ya penzi ni kwenye ndoa. Kuna uwezekano mkubwa sana wa kushushwa thamani baada ya kutoa penzi. Wanaume wengi huanza kuwa wasumbufu (kama ni kasumba yao) kwa wapenzi wao baada ya kutoka nao kimapenzi.
Pamoja na kwamba ni tendo la furaha lakini kwa mwanamke linampa unyonge na wakati mwingine huwa mwanzo wa utumwa wa mapenzi kwa kuogopwa kuachwa wakati tayari ameshatumika!
Hebu jiulize; utatumia/utatumika kwa wangapi? Ukifikiri kwa makini juu ya jibu la swali hili bila shaka utabadilisha mtazamo wako.

(ii) Hupunguza msisimko
Penzi la kienyeji mara nyingi hata wahusika huwa wanajua kabisa kuwa wanakosea. Makosa haya husababisha kupoteza msisimko wa ndani. Ni jambo la kisaikolojia sana na huenda muathirika asigundue tatizo hili kupitia dalili za kitaalamu atakazozionesha.
Mkishaibana huko nje huwa kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kupoteza msisimko wa kawaida. Mfano mawasiliano hupungua, hamu ya kuonana inapungua sana n.k
Hapa nisipoteze muda sana, wengi mnafahamu inavyokuwa; MWANAUME AKISHATEMBEA NA MWANAMKE, TARATIBU ATAANZA KUJIWEKA PEMBENI. Kama alikuwa anapiga simu mara nne au tano kwa siku, hupunguza idadi na wakati mwingine hupitisha siku nzima kabisa.
Mbaya zaidi, unaweza kumpigia wewe na bado asipokee, ukituma ujumbe mfupi hatajibu au atachelewa. Kesi nyingi sana nilizokutana nazo za wanawake wanaolalamika wapenzi wao kubadilisha utaratibu wa mawasiliano, baada ya kuwahoji walisema jambo hilo limejitokeza baada ya kuwapa penzi.

MUHIMU KWAKO KUJUA
Mwanaume wa aina hii ni yule ambaye hakuwa na mpango wa ndoa baadaye au hakuwa na uhakika na aina ya uhusiano anaotaka kwa mwanamke wake.
Sasa jiulize, ikiwa alikuwa kwenye majaribio, utajaribiwa na wangapi? Tumia hekima rafiki yangu ili kujinasua katika mtego huu.

(iii) Upungufu
Ukishautoa mwili wako kwa mwanaume, kama ni aina ya wale ambao huchunguza sana ni rahisi kukutoa kasoro. Utamsikia akisema, aaah! Huyu mwanamke bwana ana sijui nini...hakuna hoja za maana.
Kikubwa unachotakiwa kuelewa hapa ni kwamba kuutoa mwili wako hovyo kunakupeleka kwenye kujichoresha na pengine kama umekutana na mwanaume kicheche ataishia kukutumia na kukuacha kama alivyokukuta!

(iv) Msimamo
Pamoja na kwamba wanaume wengi ndiyo hasa wanaokuwa wa kwanza kushawishi kupewa mapenzi, ukweli ni kwamba ni wepesi wa kulaumu (vipengele vilivyopita nilikazia zaidi) na kuwaona wenzi wao hawana msimamo na maisha yao.
Kukuweka kwenye kundi hilo kutakukosesha nafasi ya uhakika ya kuingia kwenye ndoa, maana wengi wanapenda kuwa na wenzi wenye msimamo thabiti.

(v) Mimba
Kuna suala la mimba. Nimekutana na kesi nyingi sana za aina hii. Wanaokutana kimwili na wenzi wao bila mpangilio huwa hawazingatii sana suala la mimba lakini inapotokea ndiyo huanza kuhangaika kutafuta ushauri.

(VI) Magonjwa
Kuharakia mapenzi kuna matatizo mengi. Ukiacha kuwa katika hatari ya kupata magonjwa ya zinaa pia kuna suala la ujauzito. Mathalan utakuta msichana amepata mimba isiyotarajiwa, anatafuta shotikati na kwenda kuitoa, hapo kuna matatizo mengine mengi anayoweza kuyapata kutokana na kitendo hicho.
KUWA MSHAURI
Nataka niseme wazi kabisa kwamba, wasichana wengi hujidharau na pengine huhisi kuwa hawawezi kuwa na mawazo mazuri kwa wenzao. Sikia nikuambie; kama kuna jambo lenye thamani katika maisha ya uhusiano ni pamoja na kusaidiana mawazo.
Wakati mwingine msichana anaweza kuwa na mawazo mazuri lakini akaogopa kuyatoa kwa sababu tayari yeye si wa thamani tena. Mfano, wasichana wengi wanapenda sana kupiga ‘mizinga’ kwa wapenzi wao, wengine ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kuanzisha uhusiano. Ukiwa namna hiyo huwezi kuwa na thamani.
Nimekutana na kesi nyingi sana za namna hiyo. Wapo wanaoomba ushauri kuwa wapenzi wao hawawatunzi, wakiomba pesa hawapewi, kwani siku zote kabla yake ulikuwa unaishi vipi? Jifunze kuishi kwa kujitegemea.
Mwanaume anakuwa na amani zaidi kama akitoa fedha au kumsaidia mpenzi wake kwa uamuzi wake – siyo kuombwa. Tafsiri inayokuwa nyuma yake ni kuhonga. Kama anakuhonga ana haja gani ya kukuweka kwenye ratiba zake za mbele?
Kwa hakika hawezi kuwa na sababu hiyo. Ili kuepusha yote hayo na kujiweka katika nafasi ya kuwa mshauri wake mkuu, badilisha tabia yako. Jambo hili ni vyema likaanzia mwanzo kabisa wa uhusiano.
ACHA MAISHA YA VIFICHO
Baadhi ya watu wanapenda kufanya mambo yao gizani. Anaishi maisha ya kificho na wakati mwingine anadanganya maisha yake halisi na kuonesha picha nyingine kabisa mbele ya mpenzi wake. Hili ni tatizo.
Mwanaume ukianza kuonesha dalili kwamba penzi lenu ni la siri au unaficha ukweli wa familia yako nk, anakutoa thamani. Mwoneshe mwenzako ulivyo. Usifiche mambo yako. Mathalani una tatizo fulani la kimaisha, usimfiche, mwambie mapema.
Kumwambia kutamfanya kwanza aone unampenda, humfichi na una malengo naye ya baadaye. Ni wazi kwamba kama ungekuwa humpendi na huna malengo naye ya baadaye ungemficha maisha yako.
Kuwa wazi kutamfanya akupandishe thamani maradufu akijua kuwa amekutana na mtu sahihi. Jitahidi kuwa wazi kwa kadiri uwezavyo ili uendelee kujipandisha thamani zaidi na zaidi.
MSAIDIE
Kipengele muhimu ambacho hudhihirisha mapenzi ya dhati na kuingia ndani kwa haraka zaidi ni kusaidiana. Yapo mambo mengi ya kusadiana lakini najua wengi mmekwenda moja kwa moja kwenye fedha.
Msaada au kusaidiana siyo kwenye fedha pekee. Kati ya mambo ya msingi zaidi ya kumsaidia mwenzako ni pale anakupokuwa mhitaji. Mathalani anaweza kuwa na tatizo na fedha, lakini lazima ujiulize ni kwa ajili ya nini?
Usije ukampa fedha ya kwenda disko au kulewa baa ukadhani utakuwa umejipandisha thamani, la hasha! Nazungumzia juu ya mambo ya msingi kabisa ambayo mwenzako atayakumbuka siku zote na kukuzidishia thamani yako.
Jitahidi kumsaidia kadiri unavyoweza utakuwa juu kithamani, si tu kwamba ataona penzi lako la dhati kwake bali pia atafahamu kuwa mwanamke aliyenaye si wale wa kusubiri kupelekewa tu!
SASA UNAWEZA KUJIWEKA KATIKA KILELE CHA THAMANI
Vipengele vilivyopita bila shaka vimekupa mwanga mpya katika maisha yako ya kimapenzi. Sina shaka sasa kwamba, utakuwa umejiweka katika kilele cha thamani. Mpenzi wako hawezi kukudharau na atajua anaishi na mwanamke sahihi.



 

Copyright © 2009. MCHAMBUZI - Haki zote zimehifadhiwa