MSICHANA WA MIAKA 10 WA KIKATILI NA MWILI WAKE KUTUPWA CHOONI
MKAZI wa Kijiji cha Msanzi wilayani Kalambo katika Mkoa wa Rukwa , Festus Sungura (37) anadaiwa kumuua kikatili msichana Janeth Mwanandenje (10) na kisha kutumbukiza mwili wake ndani ya shimo la choo.
Inadaiwa choo hicho kilikuwa kikitumiwa na mkewe waliyetengana naye na lengo lilikuwa aweze kukamatwa na kufungwa kwa kosa la mauaji. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Jacob Mwaruanda alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alibainisha kuwa lilitokea Oktoba 18 mwaka huu saa 11 katika Kijiji cha Katuka Kata na Tarafa ya Matai wilayani Kalambo.
Mwaruanda alidai Oktoba 13 mwaka huu saa mbili usiku Janeth (marehemu) alikwenda kwenye ukumbi uliokuwa ukionesha mikanda ya video katika Kijiji cha Msanzi na hakurudi tena nyumbani kwao hadi mwili wake ulipogunduliwa ndani ya shimo la choo, kijiji jirani cha Katuka .
Inadaiwa siku iliyofuata, baba mzazi wa marehemu huyo aitwaye Mussa Mwanandeje , alitoa taarifa Kituo cha Polisi cha Matai ya kupotea kwa binti yake huyo.
Kwa mujibu wa Mwaruanda, Oktoba 18 mwaka huu jirani wa wazazi wa marehemu huyo katika Kijiji cha Msanzi, aitwaye Festus Sungura (37), alikwenda Kijiji cha Katuka, ambacho ni jirani na kijiji cha Msanzi.
Alikwenda kumfuata mkewe Rosemary Arusha, ambaye alirudi kwao kijijini hapo baada ya kugombana na mumewe huyo miezi kadhaa iliyopita.
Baada ya Sungura kufika Katuka, alikutana na binti yake aitwaye Digna Sungura (15), ambapo alimhoji iwapo mama yake mzazi ( mke wa Sungura) akifungwa, kwa kuwa anamchukia yeye baba yake, ataenda kuishi kwa nani? Binti yake huyo, alimjibu kuwa ataishi na bibi yake kijijini hapo Katuka.
Ndipo Sungura alipomwagiza binti yake huyo, akamwambie mama yake atoe miti mitatu, iliyowekwa juu ya shimo la choo wanachotumia, waone alichofakifanya yeye.
Mama ya binti huyo, alitoa taarifa kwa viongozi wa kijiji hicho cha Katuka, ambapo kwa kushirikiana na wakazi wengine, walitoa miti chooni hapo na kuuona mwili wa marehemu uliotumbukizwa humo.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, mtuhumiwa huyo ameshakamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani upelelezi wa shauri lake utakapokamilika.