Pata Habari Motomoto kwa kuandika E-mail yako hapo chini.


Home » » KUOLEWA SIO KILA KITU DADA....VUTA SUBIRA

KUOLEWA SIO KILA KITU DADA....VUTA SUBIRA

 
 
Ni mada ambayo imezaliwa kutoka katika mazungumzo na msomaji wangu kwa njia ya simu. Alinipigia na kuniomba ushauri juu ya tatizo lake, lakini katika maongezi yangu na yeye alionekana kuwa tayari kuendelea kuteswa, kuumizwa, kunyanyaswa katika uhusiano alionao, eti kwa sababu anaogopa kuishi bila mume.

Anataka kuolewa maana anaamini kwamba kutokuolewa ni nuksi! Masikini, alikuwa anawaza tofauti sana. Nilizungumza naye kwa muda mrefu, mwisho akaonekana kuingiwa na kitu fulani cha tofauti. Kilichobaki ni yeye kufanyia kazi ushauri niliompatia.

Hapa nimeona ni vyema kuandika, ili kwa rafiki zangu wengine wenye mtazamo kama wa dada yetu huyo, wabadilike. Naam! Ukimaliza kusoma hapa lazima utabadilika. Twende kwenye mazungumzo yangu na msomaji huyo, ambayo bila shaka yatakupa mwanga wa kuendelea na mada hii vyema.

Alisema yupo kwenye uhusiano na mwanamume ambaye kwake ni kero. Anaeleza kwamba, mpenzi wake huyo ana umri wa zaidi ya miaka 45 na yeye ana miaka 32, wakiwa katika uhusiano huo kwa zaidi ya miaka minne sasa.

Hata hivyo, alisema tatizo kubwa linalouyumbisha uhusiano wao ni kitendo cha mwanamume huyo, kuwa na tabia za kuwatongoza wadogo zake ambao anaishi nao nyumbani kwake. Baada ya kero hizo kuzidi, dada huyo aliona ni bora kuachana naye. Akamweleza mwanamume huyo msimamo wake na kuachana.

Kilichomfaya anipigie simu ni juu ya jamaa huyo kumsumbua kila wakati, akitaka warudiane. Amekuwa akiomba msamaha na kuahidi kwamba hatarudia tena. Alisema, hii siyo mara yake ya kwanza, kwani mara nyingi amekuwa akiwatongoza hata rafiki zake wa karibu na akishtukia mchezo, kazi yake imekuwa kuomba msamaha akiahidi kutorudia lakini baada ya muda, mambo yanakuwa vile vile!

Kinachomuuma zaidi ni kwamba, amejikuta akimpenda sana mwanamume huyo na anashindwa kumuondoa kichwani mwake. Nilizungumza naye juu ya tatizo lake, lakini niliona yawezekana kabisa kuna wengine wengi wenye tatizo kama hilo, lakini hawajui cha kufanya. rafiki zangu, hapa nitakupa njia madhubuti za kutumia ili uweze kukabiliana na tatizo hilo katika uhusiano wako.

Je, upo katika uhusiano na mpenzi ambaye haishi kuwatongoza rafiki, ndugu au watu wako wa karibu? Hapa haijalishi jinsia, nazungumza na wake kwa waume. Dawa hii hapa...

ANABADILIKA?
Siku zote katika uhusiano wowote ule, suala la msamaha ni jema na lenye nafasi kubwa ya kuboresha uhusiano, lakini kabla ya kuchukua hatua ya kusamehe ni lazima ujiulize, anaweza kubadilika?

Hili linaweza kudhibitishwa na historia yake ya nyuma. Haiwezekani ikawa ndiyo mara yake ya kwanza kukosea, lazima atakuwa ameshakukosea mara nyingie huko nyuma.

Je, hili ni kosa lake la kwanza? Alivyokosea huko nyuma aliomba msamaha? Kama aliomba, alirudia tena? Maana kama mtu anakosea kosa lile lile zaidi ya mara tatu na anaomba msamaha akiahidi kubadilika na habadiliki, ujue kwamba si rahisi kubadilika tena!

Lazima ujiridhishe kwamba ni kweli atabadilika na hatarudia tena. Kama nilivyosema hapo juu, utapata ukweli huu kupitia historia yake ya nyuma.

LINGANISHA UMRI NA MAKOSA
Rafiki zangu, kuna aina ya makosa fulani, ukishavuka umri fulani unakuwa huwezi kuyafanya tena, kwa mfano, kesi za kwenda disko na demu mwingine, kwa mwanaume wa miaka 45 huwezi kuzisikia tena.

Sasa hata katika hili, lazima uangalie umri wake kama unafanana na kosa lake. Unajua, kuna tabia nyingine hubadilishwa na wapenzi na nyingine ni za kuzaliwa ambazo kwa hakika huwezi kufanya mabadiliko.

Suala la kubadilisha wapenzi, linaonekana kuwa fasheni zaidi kwa vijana, lakini kama umri wake umeshasonga na bado akawa na tabia hizo, ujue kwamba hiyo ni tabia yake ya asili ambayo haibadilishiki!

Mwanaume wa miaka 52 bado unakimbikizana na vitoto vidogo, lazima kuna tatizo. Wataalamu wa Saikolojia ya Uhusiano na Mapenzi wanaamini wanaume wenye uwezo wa kuwa na familia bora na kuisimamia vyema ni wale wenye zaidi ya miaka 35, kwamba atakuwa ameshapitia mambo mengi na sasa anatamani kuwa baba tu!

Fungua ubongo wako, msimamizi wa familia hawezi kuwa malaya, anatakiwa awe mwenye kujiheshimu. Huyu anafaaa? Wa nini? Akili kichwani mwako.

NI WA MAISHA?
Lakini pia, kabla hujachukua uamuzi wa kuachana naye, lazima ujiulize swali hilo hapo juu, ni mwenzi sahihi wa maisha yako yote? Lazima awe na sifa zitakazomfanya apewe kofia ya mwenzi sahihi.
Tuliona jinsi msomaji aliyewasiliana nami, akiomba ushauri, jinsi ambavyo alikuwa akiteswa na mtazamo wa kwamba kuolewa ni kila kitu, hivyo kujikuta akiwa tayari kuendelea kuteswa na mwanamume wake ambaye ana tabia za ovyo ili kutetea kuolewa!
Sasa tuendelee na vipengele vilivyosalia...

KUTOKUOLEWA NI NUSKI?
Moyo unatudanganya sana rafiki zangu, lakini kumekuwa na mawazo mengine ya kitumwa yanayotawala hisia zetu bila kujua. Eti mtu anafikiria kwamba, kukaa bila kuolewa ni nuksi! Unajua kinachotokea? Anakubali kuwa na mwanaume yoyote hata kama ana matatizo, ili awe ameondoa nuksi.

Kama una mtazamo huo, futa. Jipe moyo dada yangu, huna nuksi. Tulia, pima mambo, kisha panga maisha yako ya baadaye. Kama mumeo yupo basi yupo tu, ni siku ya kukutana tu, ndiyo haijafika.

UNAFIKIRI HUVUTII?
Huu ni mtazamo tasa uliopo vichwani mwa wanawake wengi, hawajiamini. Wanadhani wao si wazuri au hawavutii, kwahiyo wanapokuwa na mwanaume, wanahisi kama wamebahatika tu, hivyo hawataki kuachia bahati hiyo! Huko ni kujidaganya.

Wapo wanaoshinda kwenye vioo wakijitazama na kuhakikisha kama kweli ni wazuri, kwa bahati mbaya vioo huwapa majibu tofauti kidogo...kwamba si wazuri kiivyo! Halafu kuna hizi filamu na video za wasanii wa Kizazi Kipya, basi kutwa nzima mwanamke anashinda akijifananisha na msanii fulani kwenye sinema.

Akiona aina ya wanawake wanaosalitiwa kwenye ndoa za kwenye hadithi za sinema au nyimbo za wasanii husika, hujifananisha nao! Si kweli. Wewe ni mwanamke mzuri, ambaye unapendeza kwa mwanaume wako atakayekupenda. Si rahisi kupendwa na kila mtu. Unaweza kuambiwa na mpenzi wako anakupenda, lakini mtu mwingine akashangaa, kwanini mwenzi wako anakupenda!

Kila mtu ana mzuri wake jamani. Hata hivyo, ili uwe mzuri ni lazima kwanza uanze kwa kujikubali wewe mwenyewe. Kwamba wewe ni bora, unavutia na umeumbwa kipekee. Unajua ukianza kuwaza hivyo, hata tembea yako itakuwa ya kike na kujiamini, utavaa vizuri na kujipamba sawasawa. Utavutia zaidi ya unavyofikiria.

KUOLEWA SI KILA KITU!
Kitu kibaya kingine kinachofikiriwa na baadhi ya wanawake ni kwamba kuolewa ni kila kitu! Mwanamke akishaolewa anakuwa amemaliza kila kitu. Hili si wazo baya sana, maana heshima ya mwanamke ni kuolewa.

Lakini vipi kama utaolewa na mwanamume ambaye si sahihi, akutese, akutukane, akupige, akusimange na kukufanyia kila aina ya vitu vibaya? Si utakuwa mwanzo wa kuharibu maisha yako?

Heshima ya ndoa ni kuishi kwa amani na furaha, hapo utakuwa umekamilisha kipengele hicho sawia. Kama kijisehemu hicho hapo juu kinavyosema, ni bora kuandaa maisha yako mwenyewe, uwe na uhakika na kesho yako, ukiweka malengo na kuyatimiza taratibu, ili uwe mwanamke bora. Kuwa mwanamke bora ni mwanzo wa kuelekea kuwa MKE BORA.

RUHUSU MAUMIVU MARA MOJA
Inawezekana kichwani mwako kuna mambo mengi, likiwemo la mapenzi ya dhati kwa mwanamume wako, lakini tayari amepoteza sifa za kuwa mume sahihi, uendelee kuwa naye? Hata kama unampenda sana, moyo unakusisitizia hivyo, lakini tayari taa nyekundu inawaka mbele yako.

Fanya maamuzi, bora uruhusu maumivu mara moja halafu ufurahi milele, maana kukubali machozi ya mara moja na kuachana na mtu ambaye ni kikwazo kwako, kutafungua mlango wa aliye bora kuingia. Utaonekana vipi kama hutoki nje?

KUANZA UPYA SI UJINGA
Kuanza upya si ujinga! Hakuna uwendawazimu wowote katika kuanza upya hasa unapogundua kwamba kuna makosa uliyoyafanya. Inaaminika kwamba anayekubali kukosea na kutaka kuanza upya, huwa bora zaidi katika hicho anachorudia, maana tayari anakuwa ameshajua kosa lake.

UMENIPATA?
Naamini umeelewa mada na una kitu cha kufanya. Ni bora uelewe na uanze kupiga hatua ya kuanza maisha mapya yenye mtazamo mpya. Nina hakika utakuwa umefungua ukurasa mpya wa maisha yako ya uhusiano ukiwa na furaha na nguvu mpya. Wewe ulikuwepo kabla ya mapenzi, kwa nini yakutese? Yatawale!

Mapenzi yana wigo mpana yatizamwe kwa jicho la tatu
KAMA ilivyo ada tumekutana tena kwenye kona yetu, kwa uwezo wa Karima nina imani mu wazima wa afya njema. Siku zote sitaki kupiga porojo zaidi ya kuweka mada mezani ili kila mmoja aisome.

Kumekuwa na uwezo mdogo wa watu kufikiri mapenzi ni nini na muonekano wa mapenzi uko vipi. Leo nimelenga kwenye upungufu mkubwa katika utengenezaji wa filamu zetu zinazohusu mapenzi.

Wengi wanaamini kunyonya midomo ndiyo kuwakilisha mapenzi, mtu kukaa nusu utupu kitandani au bafuni, watakuwa wametimiza lengo lao hilo.

Ndiyo maana maandalizi ya mapenzi au muonekano wa mwanamke kwa mpenzi wake huwa jambo la siri lisilotakiwa mwingine alione. Naweza nisiwalaumu waandaaji kwa vile ni uwezo wa ufahamu kuhusu mapenzi yana mtazamo gani mbele ya jamii.

Nimekuwa mfuatiliaji wa filamu nyingi za mapenzi, ndani na nje ya nchi na kuangalia maigizo ya maudhui hayo yanawakilishwaje. Je, haya mapenzi tunayoigiza ndiyo tunapaswa kuishi ndani ya familia zetu?

Inawezekana wengi hawaelewi maigizo yanayoonekana mbele ya jamii huwa kivuli cha maisha tunayoishi, mengi yakiwa yanalenga kuelimisha jamii na si kupotosha.
Pia yanazingatia utamaduni wa nchi yetu husika, lakini kwa baadhi ya waigizaji wetu nina imani kabisa ni uwezo mdogo wa kukifahamu kile unachokifanya kwa kuamini wapo sahihi na hawataki kujifunza.

Siku zote usipotaka kujifunza na kubadilika utajiona unakwenda mbele na mwisho wake utakuwa unapiga ‘maktaimu’ na kupoteza nguvu zako.
Sitaki kuhamia sana katika uwezo wa waandaaji wa maigizo ila nataka nitoe elimu ya mapenzi ambayo huenda itakufumbua macho zaidi na kuvaa uhusika ambao utaangaliwa na rika zote.

Katika maigizo hayo kuna aina nyingi ya kuwakilisha mapenzi ya wawili na si lazima mlale kitandani mkiwa nusu utupu, kunyonyana ndimi au kushikana maeneo ya aibu ambayo anatakiwa kuyagusa mtu wako tena mkiwa faragha.

Kumbuka mwanadamu ameumbwa kwa matamanio hasa kiumbe wa kike, kuna sehemu anatakiwa kuguswa na mpenzi wake tena kumuandaa kwa ajili ya tendo wkiwa faragha.

Unapocheza filamu ya mapenzi halafu mnyonyanye ndimi tena kwa kurudia zaidi ya mara tatu, inakuwa si sawa kwa vile kuna siku mzazi wa mmoja ama wahusika wote ataona mchezo ule pengine na akiwa na familia, kisha amuone mwanaye katika tukio lile.

Nasema haya kutokana na baadhi ya watu kushindwa kuwapa ruhusa wake au marafiki zao wa kike kwenda kushiriki kwenye tasnia hiyo kutokana na kile kinachofanyika huko.

Hebu tuangalie picha za nje za mapenzi hata za Kinigeria kama My love, True Love, Real Love, na za nje kama La Muja, Timeless nyingine kadhaa za Kihindi ambazo zinatazamwa kwenye ulimwengu wa filamu za mapenzi, huwezi kuona uchafu kama unaofanywa na baadhi ya waigizaji wa Tanzania na kwingineko.
Hisia unazitekaje kwa mpenzi wako?
NAAMINI rafiki zangu wote mtakuwa wazima wa afya njema, kama mimi na mpo tayari kuanza darasa hili jipya baada ya kumaliza somo lililopita last week. Karibuni tujifunze pamoja na ninaomba utayari wako ili uweze kuingiza kitu kipya ubongoni mwako.

Mara nyingi nimekuwa nikisisitiza kwamba, mapenzi ni furaha na kama upo kwenye uhusiano ambao una mateso na kila aina ya matatizo, basi ujue kwamba haupo sahihi. Hakuna masimango kwenye mapenzi, kunyanyasana na maumivu.

Tafsiri hasa ya mapenzi ni upendo, sasa kama ndivyo, si sahihi kuwa kwenye upendo, halafu chuki inachanganyika ndani yake. Hayo niliyoyataja hapo juu, mama yake ni chuki! Ndugu zangu, nirejee kusema tena kwamba uwanja wa huba ni mpana sana na unahitaji elimu kila wakati.

Wakati naandika mada hii ofisini, nilipata ugeni wa dharura. Nilipigiwa simu kutoka Mapokezi na kuelezwa kwamba nina wageni muhimu sana wanaonihitaji. Niliacha kwanza kuandaa mada hii na kuagiza waingizwe kwenye chumba cha mahojiano, kisha nikaenda.

Walikuwa wasichana wawili, ambao walionekana kuwa ni marafiki. Kwa kawaida huwa nakutana na wasomaji wangu (kwa mambo ya ushauri) kila Jumapili kwa kuweka ahadi maalumu, hivyo ujio wao haukunifanya nihisi kwamba walikuwa na shida ya mambo ya mapenzi.

Kwa haraka nikajua kwamba walikuwa na mambo mengine ya kihabari, lakini nilipowauliza, wakasema kwamba mmoja wao alitaka kuzungumza nami kwa kuwa alikuwa na hali mbaya sana katika uhusiano wake. Nikawapa utaratibu kuwa waje kuniona Jumapili (keshokutwa).

Pamoja na kuwapa utaratibu huo, waliomba sana kuzungumza nami kwa vile, mmoja wao alikuwa na tatizo kubwa. Haikuwezekana, nikamshauri nimpatie namba yangu maalumu ambayo angenipigia kwa muda niliompangia, hapo akasema: “Simu? Sawa, lakini tatizo ni kwamba ukinipigia atapokea... (mpenzi/mchumba/mume wake) simu yangu amei-divert kwake. Mh!

Anyway, nitakupigia huo muda.”
Tukaachana kwa ahadi kwamba angenipigia siku hiyo kwa muda ambao tulikubaliana.

TUNAJIFUNZA NINI?
Pamoja na kwamba sikuweza kuzungumza naye chochote mpaka naandika mada hii, niligundua mengi sana kutoka kwa dada yule ambaye kwa haraka nilimkadiria kuwa na umri kati ya miaka 22-28.

Ni msichana mrembo kwa kumtazama, lakini uso wake umepoteza matumaini. Anaonekana yupo kwenye uhusiano ambao kwake ni mateso. Nathubutu kusema kwamba, inawezekana kabisa yupo kwenye mapenzi ya utumwa.

rafiki zangu, inapofikia hatua mpenzi wako hakuamini kiasi kwamba ana-divert simu yako kwake, ujue hapo kuna tatizo. Niliagana na dada huyo nikimpa matumaini makubwa kwamba, tatizo lake lingeisha kwa kuwa hakuna kisicho na dawa.

Nilimwambia: “Samahani nashindwa kuongea na wewe sasa hivi kwa kuwa ni nje ya utaratibu, lakini pia nina majukumu mengi yanayonisubiri, ila nakuhakikishia tatizo lako limefika mwisho. Kwa kuwa umeonana na mimi, amini masaibu yako yameshapata dawa!”

Nashukuru aliondoka akitabasamu kidogo. Nilikuwa na matarajio makubwa ya kumpa dawa ya tatizo lake. Wiki ijayo nitawaletea mrejesho. Rafiki zangu, niliona hili liwe kama utangulizi wa somo letu.

HISIA NI NINI HASA?
Katika tafsiri ya kawaida hisia ni neno linalotokana na hisi, fikiri, buni. Kwenye uwanja wa mapenzi linanyambulishwa tofauti kabisa. Huku linajulikana kama mshawasha, mhemko, miliki n.k.

Kwa kifupi, hakuna tafsiri ya moja kwa moja ya neno hilo, lakini limebeba ile hali ya mwenzi kuwa na hamu, mapenzi, uhitaji zaidi kwa mwenzake. Ndiyo maana mtu anaweza akauliza, “Nitawezaje kuteka hisia za mpenzi wangu?”
Bila shaka tupo pamoja.

UNAZITEKAJE?
Hapo ndipo kwenye tatizo kwa watu wengi walio kwenye uhusiano. Wapo wasioweza kabisa kuteka hisia za wapenzi wao. Hawajui mbinu za kufanya hivyo. Rafiki zangu, suala la kumfanya mpenzi wako akupende, awe na hamu na wewe, akufikirie, asiwaze kukusaliti lipo mikononi mwako.

Ni kazi yako. Hapo unaanza na kujua ni mambo gani ambayo hayapendi na yapi anayapenda. Kujua jambo hilo, unakuwa unaelekea kwenye kuelewa namna ya kumaliza kabisa tatizo hilo.
Kuna ambao wapo kwenye uhusiano, halafu wanashangaa ghafla wapenzi wao wamebadilika.

Wanakuwa wakali bila sababu, wakorofi, hawana hamu ya kukutana nao faragha na mengine. Umewahi kujiuliza kwa nini? Jibu ni rahisi sana, AMEPOTEZA HISIA KWAKO!
Kama ndivyo, kazi ipo mikononi mwako ya kurejesha hisia hizo kama zamani. Yapo mambo mengi ambayo natakiwa kuzungumza na wewe kuhusu namna ya kurejesha hisia za mwenzi wako kwako. Ni rahisi sana, wiki ijayo nitakuletea.

Kitu kikubwa rafiki yangu, ninachotaka kukuacha nacho ni kwamba, matatizo mengi kwenye uhusiano husababishwa na kupoteza hisia. Mchunguze mpenzi wako, siku hizi anakukaripia? Anakusimanga? Hakusikilizi?

Anakudharau? Hapendi kukushirikisha kwenye mambo yake? Kama una matatizo haya ujue chanzo chake ni kupoteza hisia. Kazi yangu mimi ni kurejesha amani katika uhusiano wako.
 

Copyright © 2009. MCHAMBUZI - Haki zote zimehifadhiwa