MWAKA  2005 nilikuwa nikipanda daladala na Naseeb Abdul (Diamond) katika kituo  cha Shule Tandale Magharibi jijini Dar es Salaam. Wakati huo, sikuwa  hata na wazo kwamba atakuja kuwa mtu maarufu katika muziki hata  kushughulisha watu kutaka kujua zaidi kuhusu maisha yake. 
Baada ya hapo nikaanza kuona wimbo wake wa kwanza kwenye video, ‘Nenda Kamwambie’ kilikuwa kibao kizuri kilichompa umaarufu, ndipo alipoanza kunivutia kusikiliza nyimbo zake. Baada ya video ile sikumuona tena kituoni kama ada yetu, nikaanza kusikia anaendesha gari aina ya Toyota Celica.
Kutoka mwaka 2006 mpaka sasa ni mfululizo wa mafanikio aliyoendelea kuyapata kijana huyu aliyezaliwa Septemba 28, 1988 mpaka kuwa mwanamuziki wa kwanza Tanzania kulipwa pesa nyingi kutokana na shughuli hiyo.
Kutokana  na utafiti uliofanywa na tovuti inayozungumzia masuala ya vijana  inasemekena ‘Diamond Platnamz’ anapata kiasi cha Sh Mil 16 kwa matamasha  mawili anayofanya katika mwezi.
Mbali ya mikataba minono aliyoingia na makampuni mbalimbali yanayonufaika kwa taswira ama sauti ya mwanamuziki huyo kijana, Diamond anaingiza fedha nyingi kila anaposafiri nje ya Tanzania na bara la Afrika kufanya matamasha ya muziki.
Mbali ya mikataba minono aliyoingia na makampuni mbalimbali yanayonufaika kwa taswira ama sauti ya mwanamuziki huyo kijana, Diamond anaingiza fedha nyingi kila anaposafiri nje ya Tanzania na bara la Afrika kufanya matamasha ya muziki.
 Wakati  Diamond, ambaye hajatimiza hata miaka kumi kwenye tasnia ya muziki kuna  mtu mmoja anaitwa Muhidini Gurumo, amejishughulisha na muziki kwa  takriban miaka 45 lakini kila alipokutana na swali hili kutoka kwa  wanahabari kuwa kwa kipindi chote hicho muziki umemsaidia nini, jibu  lake ni: “Bado hakuna ninachoweza kujivunia kupitia muziki, hali ya  maisha ni ngumu.”
 Gurumo  ambaye alizaliwa 1940 alianza muziki mwaka 1959 akiwa na bendi ya  Kilimanjaro Chacha Band. Sasa ni takriban miaka 45, umri wa baba mwenye  wajukuu lakini alichofanikiwa ni kujenga nyumba mbili na kupata shamba  moja. Gari lenyewe alizawadiwa na Diamond mwaka huu baada ya kulalamika  sana kwenye vyombo vya habari.
 Nini Tatizo
 Maalim  Gurumo (Kamanda), analalamika kuwa wanamuziki wa kizazi kipya  wanasifiwa sana na vyombo vya habari. Akisisitiza kuwa hawana ubunifu,  nyimbo zao hazina athari katika jamii na hudumu chini ya mwaka mmoja  zinapoteza taswira.
 Lakini  amesahau kuwa wanamuziki wa sasa wengi wamejiajiri, kipindi hicho bendi  nyingi zilimilikiwa na kampuni, taasisi ama mtu ambaye anapenda sanaa  hiyo ya muziki.
 Lakini sasa wanamuziki wameamka, wanajimiliki wenyewe pesa wanazopata zinaingia mifukoni mwao.
 Mathalan  tangu Diamond aanze kuimba ameshaingia zaidi ya mikataba kumi tofauti  ambayo ilimnufaisha yeye kama Diamond, matamasha yake yanamnufaisha  yeye, kikundi anachomiliki anakilipa kiasi wanachokubaliana kutokana na  uwezo wa mwanakikundi.
Mwaka  jana, 2012, Diamond aliingia mkataba na kampuni ya I-View Studios wa  kusimamia kazi zake zote kwa miaka miwili. Huu ni mkataba ambao  umemjengea heshima kubwa sana. Ingawa kiasi cha malipo kilifanywa siri  lakini inaonekana ni mkataba mnono.
 Kampuni  nyingine ya One Touch, ilifunga naye mkataba wa kuwa wasemaji wake.  Yaani kila anachotaka kufanya ama kuzungumza kwenye jamii, ikiwa kuna  kampuni inataka kufanya naye mazungumzo ya kibiashara, One Touch Company  ndio watakaofanya kazi hiyo.
 Hilo  tu linamfanya Diamond awe na uwezo mkubwa wa kupata fedha kutokana na  muziki. Mara nyingine msanii anashindwa kujua thamani yake, anaweza  kutaja kiasi kidogo cha fedha katika ‘dili’ kubwa. Lakini kwa kupata mtu  wa kukusimamia kwenye mazungumzo ya kifedha lazima uwe tajiri.
 Aidha,  bendi ambazo Maalim Gurumo amehama kutokana na sababu za kimaslahi  hazipungui kumi, alianza na Kilimanjaro Chacha Band, Kilwa Jazz Band,  NUTA Jazz Band, Mlimani Park, Safari Sound Ochestra, Rufiji Jazz, na  nyingine nyingi kabla ya kumalizia muziki kwenye bendi kongwe ya Msondo  Ngoma Music Band.
 Kote  huko alizunguka kwa kutumia kichwa kitupu kujadili thamani ya sauti  yake, hakuwa na mshauri wa masuala ya muziki ambaye atamwambia kutokana  na thamani yako usikubali kuhama bendi hii ili kuenda bendi nyingine  bila kupewa kiasi fulani cha fedha.
 Aliweza  kuitwa baa akawa anakunywa bia na nyama choma huku anajadili  mustakabali wa maisha yake na mkurugenzi wa bendi pinzani na anayofanyia  kazi.
 Katika  mazungumzo yake na wanahabari Maalim Gurumo aliwahi kutamka kuwa  anatamani siku zirudi nyuma ili anufaike na muziki wake. Lakini nakataa,  hata awe vipi kutokana na mfumo anaoutumia hawezi kuwa tajiri kama  Diamond.
 Leo  hii, Maalim Gurumo akiandaa tamasha na kuingiza Sh Mil 50, basi  atakachoambulia ni asilimia  10 ya mapato ambayo ni Sh Mil 5, ambacho  kitakuwa ni kiasi kikubwa kuwahi kukipata kwa tamasha moja tangu aanze  kuimba.
 Lakini  siku hiyohiyo Diamond akialikwa katika tamasha hilo la Gurumo ataondoka  na Sh Mil 8 taslimu bila kupungua senti. Bado tofauti ipo kubwa.
 Aidha,  mbali ya mapato ya stejini lakini Diamond ana mikataba minono na  makampuni ya simu ambayo yanatumia nyimbo zake kama miito ya simu, ana  mkataba mwingine mnono na kampuni ya Vodacom, ana mkataba na kampuni ya  vinywaji baridi ya Coca Cola hata kufikia kujiita Coke Boy.
 Tukiwakusanya  wanamuziki wa zamani kuanzia Mbaraka Mwinshehe mpaka kufikia Maalim  Gurumo, bado hawawezi kufikia mafanikio ya muda mfupi aliyoyapata kijana  mdogo Naseeb Abdul ‘Diamond’ ambaye hata ladha ya ndoa hajaionja  kutokana na umri wake kuwa mdogo.
 Wakati  Gurumo akijisifia nyumba mbili alizojenga kwa tamu, Diamond ana nyumba  zaidi ya mbili ambapo moja amemjengea mama yake yenye thamani inayofikia  zaidi ya Sh Mil 50.
 Pengine Gurumo ni mwanamuziki bora zaidi kuliko Diamond lakini mwenziye amemzidi kwenye ujanja wa kutafuta fedha
-muhariri wa gazeti la Raia  Mwema 

