Pata Habari Motomoto kwa kuandika E-mail yako hapo chini.


Home » , » UMRI MKUBWA WAWAKOSESHA WANAFUNZI 76 WENYE VIGEZO KUJIUNGA NA KIDATO CHA 5

UMRI MKUBWA WAWAKOSESHA WANAFUNZI 76 WENYE VIGEZO KUJIUNGA NA KIDATO CHA 5

                                   Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo
WAKATI wanafunzi 34,213 wamechaguliwa mwaka huu kuingia kidato cha tano, vyuo vya ufundi vya umma na Taasisi ya Menejimenti ya Maendeleo ya Maji wanafunzi 76 wamekosa nafasi hizo kutokana na umri.
Wakati nafasi zilizokuwapo kwa ajili ya kidato cha tano mwaka huu ni 43,757 ambazo ilipaswa zijawe, kwa upande wa masomo ya Sayansi ya Jamii, nafasi nyingi zimebaki wazi bila kupangiwa wanafunzi isipokuwa za Sayansi, ambazo zimepata idadi kubwa.
Ingawa wapo baadhi ya wanafunzi ambao matokeo yao yanaruhusu kujiunga kidato cha tano, 76 hawakupangiwa kutokana na sababu kadhaa miongoni ikiwa ni umri mkubwa wa kati ya miaka 25 na 35.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akitangaza kwa waandishi wa habari uchaguzi huo wa wanafunzi kwa kuzingatia takwimu za matokeo yao katika mtihani wa kidato cha nne wa mwaka jana.
Idadi hiyo ya wanafunzi 34,213 waliochaguliwa, ni sehemu ya 34,599 wenye ufaulu bora katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa mwaka jana uliotangazwa mwaka huu.
Katika idadi hiyo, waliopangiwa kidato cha tano ni 33,683 na vyuo vya ufundi ni 530 huku ikitajwa kuwepo ongezeko la wanafunzi 2,790 wa kidato cha tano na vyuo, sawa na asilimia 8.9 ikilinganishwa na wanafunzi 31,423 waliochaguliwa mwaka jana.
Kwa upande wa waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano pekee katika shule za Serikali mwaka huu, Naibu Waziri alisema lipo ongezeko la wanafunzi 2,824 sawa na asilimia 9.15 ikilinganishwa na 30,859 waliochaguliwa mwaka jana.
HKL yakosa wanafunzi
Kwa mujibu wa Mulugo, nafasi zilizokuwapo ni 43,757 na kati yao, 18,564 ni za Sayansi na 25,193 za Sayansi ya Jamii; sawa na ongezeko la nafasi 3,757 ikilinganishwa na 41,000 za mwaka jana.
Naibu Waziri alisema nafasi zote za Sayansi zimepangiwa wanafunzi. “Nafasi zote za masomo ya Sayansi zimepangiwa wanafunzi na baadhi ya tahasusi waliopangwa ni wengi kuliko nafasi zilizopo,” alisema Mulugo.
Alitoa mfano wa tahasusi ya Fizikia, Kemia na Baolojia (PCB), kulikuwa na nafasi 6,188 na waliopangwa ni 6,400. Kwa masomo ya tahasusi za Sayansi ya Jamii nafasi nyingi zimebaki wazi.
“Kwa mfano, tahasusi ya HKL (Historia, Kiswahili na Kiingereza) kulikuwa na nafasi 5,300 lakini zilizopangiwa wanafunzi ni 1,527,” alisema Mulugo.
Wavulana wengi
Alisema kati ya waliochaguliwa kutoka shule za Serikali na zisizo za Serikali kujiunga na kidato cha tano, wavulana ni 23,383 na wasichana ni 10,300.
Wavulana 13,708 sawa na asilimia 58.62 wamechaguliwa kujiunga na masomo ya Sayansi na 9,675 Sayansi ya Jamii. Kwa upande wa wasichana, waliochaguliwa ni 10,300 kidato cha tano; kati yao, 5,038 sawa na asilimia 48.91 wanajiunga na Sayansi na 5,262 wa Sayansi ya Jamii.
Shule zaongezeka
Mulugo alisema wanafunzi hao wamepangiwa katika shule 207 zikiwamo mbili zilizoongezeka mwaka huu kwa ajili ya kidato cha tano. Nazo ni Tandahimba ya Mtwara na Miono ya Pwani.
“Kutokana na uchache wa wanafunzi wenye sifa za kujiunga kidato cha tano hasa kwa masomo ya Sayansi za Jamii, hatukuongeza zaidi shule mpya za kidato cha tano mwaka huu, bali nimehamasisha wadau katika halmashauri kuimarisha miundombinu ikiwemo maabara katika shule zilizopo na zinazotarajiwa kujengwa, “ alisema Mulugo.
Kuhusu wanaojiunga na vyuo vya ufundi na Taasisi ya Menejimenti ya Maendeleo ya Maji, Mulugo alisema idadi imepungua kutoka wanafunzi 564 mwaka jana hadi 530 mwaka huu, huku idadi ya wanafunzi wa kike ikiwa imeongezeka kutoka 47 ya mwaka jana hadi 114 mwaka huu sawa na ongezeko la asilimia 142.55.
“Ninatoa mwito kwa wanafunzi wa kike waliopo shuleni kusoma kwa bidii Sayansi ili mwakani idadi ya wasichana wanaojiunga na vyuo vya ufundi iongezeke zaidi ikilinganishwa na wavulana, “ alisema Mulugo.
Sayansi yaongoza
Aliongeza kuwa wanafunzi waliopangwa kusoma Sayansi ni wengi kuliko waliopangwa katika Sayansi ya Jamii. Alipongeza walimu kwa kuzingatia mbinu za ufundishaji Sayansi walizopata kupitia mpango wa mafunzo kazini kwa walimu wa Sayansi.
Umri wawachuja Hata hivyo, Mulugo alisema wanafunzi 76 waliokuwa na sifa za msingi kuwawezesha kuingia kidato cha tano, hawakuchaguliwa kwa sababu mbalimbali.
Miongoni mwao ni pamoja na wanafunzi 70 ambao masomo yao yalikosa mlingano wa tahasusi. Aidha wanafunzi watano walikutwa na umri mkubwa wa zaidi ya miaka 25 baada ya kubainika kuwa na miaka kati ya 28 na 35 na mwingine hakuwa raia wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Mulugo, hao wenye umri mkubwa, Sera ya Elimu hairuhusu kuwapangia kidato cha tano kwenye shule za umma isipokuwa inawapa uhuru wa kuendelea katika shule binafsi na kuwapa nafasi ya kufanya mitihani ya Taifa ya Serikali.
Shule kunyang’anyana
Wakati Serikali ikifanya uchaguzi huu, baadhi ya shule binafsi zimeshachukua baadhi ya wanafunzi kujiunga na kidato cha tano. Hali hii inadhihirisha idadi ya wanafunzi waliopangwa katika shule hizo za umma, haitakuwa kama ilivyo katika uchaguzi huu na badala yake, ama kwa shule binafsi, au za umma kutakuwapo pengo.
Ufaulu mwaka jana
Watahiniwa 431,650 walifanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana. Kati yao, idadi ya watahiniwa wa shule ilikuwa 370,837, wa kujitegemea 60,813. Waliofaulu kwa madaraja ya kwanza hadi nne walikuwa 185,940. Kati yao waliofaulu, wa shule ni 159,747 na wa kujitegemea 26,193.

 

Copyright © 2009. MCHAMBUZI - Haki zote zimehifadhiwa