Pata Habari Motomoto kwa kuandika E-mail yako hapo chini.


Home » » MKE AKAMATWA KWA KUPANGA NJAMA ZA KUMUUA MUMEWE

MKE AKAMATWA KWA KUPANGA NJAMA ZA KUMUUA MUMEWE

Mke wa ndoa wa mfanyabiashara wa madini Arusha, Jackson Manjuru, amekamatwa na Polisi kwa tuhuma za kupanga njama za kuua mumewe.

Akizungumza na mwandishi juzi, Manjuru anayeishi Moshono jijini hapa, alikiri mkewe Janet Simon, kushikiliwa Polisi kwa tuhuma hizo, huku akisisitiza haamini kama ni kweli.

“Siamini kama mke wangu wa ndoa, tena ya kikristo, anaweza kufikiria kunitoa roho eti kwa sababu ya mali… wakati nimempa kila anachohitaji duniani.

“Yote naliachia Jeshi la Polisi wafanye kazi yao bila upendeleo wala ubaguzi,” alisema Manjuru ambaye ni mfanyabiashara wa kuuza na kununua madini ya tanzanite jijini hapa na mkoani Manyara.

Awali kabla ya Manjuru kukiri mkewe kushikiliwa Polisi kwa tuhuma hizo, mwandishi alipata taarifa za ndani kutoka Polisi, zikieleza kuwa Janeth alikuwa akishikiliwa tangu Julai 19.

Taarifa hizo zilidai kuwa mke huyo anatuhumiwa

kupanga njama za kuua mumewe kwa kutumia majambazi wa kukodi, ili arithi mali.

Inadaiwa kuwa Janeth alimtumia dereva teksi, ili atafute vijana watano watakaofanya kazi hiyo, na kuahidi kuwalipa Sh milioni 30 za malipo ya awali kwa ajili ya mauaji hayo.

Kwa mujibu wa madai hayo, mmoja wa vijana hao ambaye hakutaka kushiriki masuala hayo pamoja na kuchukua Sh milioni tano za awali, alifikisha suala hilo Polisi walioweka mtego wa kuwanasa wahusika na Janet.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Liberatus Sabas alipopigiwa simu ya mkononi, hakukanusha wala kukiri kukamatwa kwa wahusika hao wanne, lakini akasema atatoa taarifa rasmi baada ya mahojiano na watuhumiwa hao kukamilika.

 

Copyright © 2009. MCHAMBUZI - Haki zote zimehifadhiwa