Sasa ni dhahiri kuwa maisha ya kiongozi wa zamani wa nchi hii, Nelson Mandela yamo hatarini kutokana na kwamba anaishi kwa msaada wa mashine, imethibitishwa na mmoja wa wazee wa ukoo wa kiongozi huyo.
Binti yake mkubwa Makaziwe naye amethibitisha hilo, akisema hali ni mbaya na chochote chaweza kutokea.
"Naweza kusisitiza hilo, kwamba Tata (baba) hali yake ni mbaya sana, chochote chaweza kutokea, lakini nataka nisisitize tena, kwamba ni Mungu tu ndiye anajua muda wa kuondoka,” alikiambia kituo cha utangazaji cha SAFM jana.
Hali hiyo inayotia mashaka imesababisha hata Rais Jacob Zuma afute safari yake ya Msumbiji ambako alipanga kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
“Ndiyo, anatumia mashine kupumua,” Mzee Napilisi Mandela aliiambia AFP muda mfupi baada ya kumtembelea Mandela hospitalini juzi. “Hali ni mbaya, lakini tutafanyaje.”
Zuma alifuta safari yake iliyokuwa ifanyike jana baada ya “kubaini, kwamba kiongozi huyo wa zamani hali yake bado ni mbaya,” taarifa kutoka Ofisi ya Rais ilisema.
Wakati huo huo, kiongozi wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu Ban Ki-moon alisema juzi kwamba dunia yote inamwombea Mandela wakati huu ambapo anapigania maisha yake.
Ban alimwita Mandela “mmoja wa mashujaa wa karne ya 20” katika hafla ya kuadhimisha miaka 50 ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU (sasa Umoja wa Afrika-AU) iliyofanyika New York, Marekani, ambao uliongoza mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.
“Najua fikra na maombi yetu viko na Nelson Mandela, familia yake na wanaompenda, Waafrika Kusini wote na watu wote duniani ambao wamekuwa wakivutiwa na matendo yake maishani na kuwa mfano wa kuigwa,” alisema Ban.
“Hebu nasi leo tuoneshe dhamira ya uwajibikaji wa dhati katika kuhakikisha tunaboresha maisha na fursa za Waafrika wote,” alisema Katibu Mkuu wa UN.
Zuma alimtembelea Mandela hospitalini juzi saa nne usiku na kumkuta akiwa bado na hali mbaya, msemaji wa Rais, Mac Maharaj alisema.
“Rais Zuma alizungumza na madaktari ambao bado wanaendelea kufanya kila linalowezekana kuokoa maisha yake ... ameamua kufuta safari yake ya Maputo kesho (jana), ambako alitakiwa kuhudhuria Mkutano wa Uwekezaji katika miundombinu kwa nchi za Kusini mwa Afrika wanachama wa SADC.”
Mandela (94) alilazwa katika hospitali ya moyo ya Medi-Clinic iliyoko hapa Juni 8 kutokana na kuibuka upya kwa matatizo ya mapafu yake.
Katika hatua nyingine, mjukuu wake, Mandla Mandela, amekanusha kuwapo kwa mvutano kati yake na shangazi yake, Makaziwe, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa jana.
Magazeti yaliripoti juzi kwamba anadaiwa alijitoa kwenye kikao cha familia kilichofanyika Qunu Jumanne.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, anadaiwa kuhamisha makaburi ya watoto watatu wa Mandela kutoka Qunu hadi Mvezo mwaka 2011, bila hata kushauriana na familia.
Iliripotiwa pia kuwa familia hiyo ilikuwa ikitaka watoto hao, Makgatho, Thembekile na Makaziwe, warudishwe Qunu.
“Chifu Zwelivelile (Mandla) hana suala lolote na mtu mwenye mamlaka ya kurudisha Qunu kaburi lolote au makaburi yote,” msemaji wa Mandla, Freddy Pilusa alikaririwa akiiambia The Star jana.
“Mvezo ndiko mahali ilikozaliwa familia ya Mandela na kimila ndiko nyumbani kwao, na hivyo ndiko iliko historia ya familia hiyo.” Alisema Mandla hawezi sasa kuzungumzia lolote kuhusu mipango ya maziko ya babu yake.
Waganga wa jadi wa Limpopo jana walifanya matambiko katika ofisi za ANC zilizoko Polokwane kumwombea Mandela.
Mwenyekiti wa Timu kazi ya ANC Limpopo, Falaza Mdaka, alisema waganga hao waliomba kufanyia tambiko lao katika ofisi hizo wakisema ndiko kulikuwa ‘nyumbani’ kwa Mandela na kuongeza kuwa alikuwa mtu wa aina yake na dunia bado inamhitaji.
Waganga hao waliimba nyimbo za mapambano na kuchoma ubani, wakiwaomba wahenga kumponesha kiongozi huyo anayependwa na nchi nzima.
“Mandela anahitaji msaada wa wahenga,” alisema mmoja wa waganga hao, Sylvester Hlathi.