Pata Habari Motomoto kwa kuandika E-mail yako hapo chini.


Home » » KUTANA NA SHUHUDA WA MLIPUKO WA BOMU AKIELEZEA MWANZO MWISHO WA TUKIO ZIMA

KUTANA NA SHUHUDA WA MLIPUKO WA BOMU AKIELEZEA MWANZO MWISHO WA TUKIO ZIMA

Mei 5 mwaka 2013 ni siku ambayo haitafutika katika historia ya Tanzania kutokana na tukio la kusikitisha la kutupwa kwa bomu kanisani, ambapo watu watatu walifariki na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa.
Tukio hilo lilitokea mbele ya Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo, Askofu Mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo Kuu la Arusha, walipokuwa wakizindua jengo la Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti, Arusha.
Siku hiyo iliyoleta historia mbaya kwa taifa letu kutokana na tukio hilo ambalo viongozi mbalimbali waliliita la kigaidi, halitaweza kusahaulika kwa baadhi ya watu ambao wanasimulia:
Fatma Tarimo (39), mkazi Olasiti mkoani Arusha. Yeye, ambaye ni mama wa watoto watano, anasema siku ya tukio aliamka asubuhi akiwa ni mtu mwenye furaha kuliko siku zote huku akiwa shauku ya kumaliza shughuli zake mapema kisha awahi kanisani.
Anasema kuwa kabla ya kujiandaa kwenda kanisani aliwatayarisha watoto wake ili watangulie.
Mama huyo ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Burka Estate, anasema baada ya watoto wake kuondoka yeye alibaki nyumbani ili kumtayarishia chakula mama yake aliyekuwa amemtembelea.
Anaeleza kuwa, baada ya kumaliza shughuli zake alijiandaa na kwenda kanisani ambapo alipata lifti ya gari la watawa wa kanisa hilo.
“Pale kuna misa mbili, siku nyingine watoto huwa wanakwenda misa ya pili, lakini siku ile kwa sababu ya ufunguzi wa jengo la kanisa kulikuwa na misa moja, mimi nikasema watoto watangulie kanisani na mimi nimtayarishie kwanza mama chakula,” anasema.
Anasema kuwa, walipofika kanisani walikaa nyuma huku mbele kukiwa na viongozi mbalimbali wa kanisa hilo, watawa, pamoja na vikundi mbalimbali vya kwaya.
Aeleza bomu lilivyolipuka
Bomu lile halikutua mbali sana na nilipokuwa, ilikuwa kama umbali wa hatua moja tu na lilipotua chini watu walisogea pembeni kidogo na eneo lile kulikuwa na watoto wengi.
Nakumbuka wakati huo misa ilikuwa inaendelea na viongozi walikuwa wamesimama tayari kwa kuzindua jengo, niliona kitu kama chuma kimerushwa kikatua pembeni mwangu.
Mwanzoni nilidhani labda ni jiwe ama kijiti watoto wamerusha, kwa kuwa sikuwa mbali na lilipotua niliweza kulichunguza.
Kilikuwa ni kitu cha chuma chenye umbo kama yai,  kwenye lile eneo jembamba kulikuwa na nyaya zenye rangi kama ya kijani na njano, hicho chuma chenyewe kilikuwa na rangi nyekundu ama shaba.
Nakumbuka kuwa kilivyotua chini watu walisogea pembeni kidogo wakawa wanakishangaa, wengine waliangalia kidogo na kupuuza wakawa wanafuatilia matukio yaliyokuwa yakiendelea mbele.
Mimi baada ya kuona halikuwa jiwe niliendelea kukitizama kwa makini, tangu kinatua chini mpaka kinalipuka, ilichukua karibu dakika moja, ndiyo maana hata baadhi ya watu walikuwa wameacha kukitizama wakawa wanafuatilia misa.
Wakati nikiendelea kukiangalia huku nikiwa sijapata jibu kuwa ni kitu gani, ulitokea mlipuko mkubwa, tulinyanyuliwa juu, kukawa na moshi mzito ulioingia mpaka kifuani nikawa siwezi hata kupumua.
Nilihisi kuna kitu kinanivuta kwenda juu, mara chini, siwezi kuhema wala kukimbia, ardhi yenyewe nilikuwa siioni, wala kukimbia siwezi.
Kwa wakati huo, hata maumivu nilikuwa siyasikii, nikataka kukimbia, ardhi siioni, ninaona tu kama napelekwa huku na huku, nikasema nitashindana na hizi nguvu mpaka saa ngapi, nikasema ngoja nitulie.
Baada ya kutulia kidogo ndipo niliona watu wamelala chini wakiwa wametapakaa damu, na mimi nikawa nasikia maumivu upande wa kulia ambapo nilikuwa nimeumia.
Kwa nini bomu lilivyotua hawakukimbia?
Anasema mama kuwa, chuma kile kilichukua muda mrefu na kwa kuwa hakuna mtu aliyewahi kuona bomu hawakuwa na sababu yoyote ya kupata hofu.
“Hata mabomu tunayoyaona kwenye televisheni huwa yanafika chini na kulipuka, lakini hili lilikaa karibu dakika moja nzima, tungejua labda tungekimbia ama kufanya kitu kingine lakini pale watu wote tulikuwa tunashangaa tu,” anasema.
Anaongeza, “Kwa kuwa ni kanisani  mtu unakuwa na amani kabisa, mpaka sasa hivi naona kama ule ulikuwa ni mchezo wa kuigiza kwa sababu ukiwa kanisani unakuwa na amani na uhuru, siamini kama vitendo vile vinaweza kutokea kanisani labda kwenye maeneo mengine ya anasa.”
 

Copyright © 2009. MCHAMBUZI - Haki zote zimehifadhiwa