Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu Suzana Lyimo (Chadema),ameitaka Serikali kuwapeleka mahakamani marais wanaoshindwa kutimiza ahadi zao hadi wanastaafu.
Lyimo alitoa pendekezo hilo jana bungeni alipouliza swali la nyongeza kuhusu ahadi za Rais Jakaya Kikwete ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wabunge wengi kutoka Chama Cha Mapinduzi.
“Mheshimiwa Spika, wabunge wengi wamekuwa wakilalamikia juu ya ahadi za Rais kila mahali na hasa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi, je inakuwaje Rais anaposhindwa kutimiza ahadi zake na wakati mwingine hadi anamaliza kipindi chake cha uongozi ni kwa nini asishtakiwe mahakamani kwa uongo,” alihoji Lyimo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisema kuwa hakuna tatizo kwa Rais kutotimiza ahadi zake kwani anapomaliza muda wake Rais anayemrithi huwa anatimiza ahadi hizo kwani ni ahadi za Rais sio anatoa fedha mfukoni mwake.
Mbunge wa Viti Maalumu Suzana Lyimo (Chadema)
Mbunge wa Viti Maalumu Suzana Lyimo (Chadema)
Awali katika swali la msingi Mbunge wa Mkinga Dustan Kitandula (CCM), alitaka kujua ni hatua zipi zimechukuliwa ili kutimiza ahadi ya Rais juu ya kujenga kwa haraka Hospitali ya Wilaya ya Mkinga.
Pia alihoji kuhusu kupandishwa hadhi Kituo cha Maramba.