Pata Habari Motomoto kwa kuandika E-mail yako hapo chini.


Home » » JE HIP HOP BILA MADAWA HAIWEZEKANI......?

JE HIP HOP BILA MADAWA HAIWEZEKANI......?

Hakika ni jambo la kusikitisha sana pale ambapo tunapowaona vijana na watu tunaowapenda wakipoteza maisha au kupotea kimuelekeo kwa sababu ya mambo yanayoweza kuepukika.
Nafahamu kwamba yapo mengi ambayo hupelekea kubomoa muelekea wa maisha ya binadamu hasa vijana, ambao ndio nguvu kazi ya maisha yao binafsi, familia zao na Serikali kwa ujumla.

Starehe zipo nyingi na hakika huwa haziishi, kama tunafahamu hilo ni kwa nini tusijaribu japo kuchagua zile zenye afadhali...?

Uvutaji wa bangi, kunywa pombe kupita kiasi, utafunaji wa mirungi na matumizi ya madawa ya kulevya ni baadhi ya starehe ambazo vijana wengi hasa wenye vipato vya wastani wamekuwa wakijihusisha navyo.

Kila kukicha ongezeko la utumiaji wa vilevi limekuwa likiongezeka na kuzidi kupunguza nguvu kazi, bila ya watumiaji kufahamu kwa bahati mbaya au makusudi juu ya madhara ya utumiaji wa vilevi hivi.

Tumeiona mifano mingi na bado kasi inaongezeka kama vile watu hawaelewi athari za madawa ya kulevya, mfano wa karibuni ni wa msanii Ray C ambaye kama si msaada wa watu akiwemo Rais Kikwete basi hakika tungeweza kumpoteza.

Kifo cha msanii Albert Mangwear  a.k.a Ngwear ni pigo kwa na pengo kwa Tasnia ya Muziki wa Kizazi Kipya na hata kwa Serikali kama moja kati ya nguvu kazi yake.

Na tujiulize je Muziki au Hip Hop bila madawa je haiwezekani...? Ni kwa nini wasanii wengi huwa wanajihusisha na madawa ya kulevya..? Kuna uhusiano gani kati ya muziki na madawa ya kulevya...? Je ukiwa mwanamuziki ni lazima uwe unavuta bangi, kunywa pombe nyingi, kutafuna mirungi au kubwia unga...?

Ni nini hasa faida yake kwenye muziki, je ndivyo ambavyo vinawapa uwezo wa kuandika mashairi au nguvu ya kuimba kwa zaidi ya saa nzima jukwaani bila kuchoka..?

Hata kama ni hivyo bado madhara yake ni makubwa ukilinganisha na faida ya ziada ambayo vijana na wanamuziki huipata kama ambavyo wengi wanavyodhania..

Najua wapo wengi wanojihusisha na utumiaji wa madawa ya kulevya na tunawafahamu na mara nyingi tumekuwa tukisema kwamba tunawapenda kutokana na kazi zao nzuri wanazozifanya.

Naamini kama kweli unampenda mtu hakika hutopenda kumuona akipotea, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha tunawasaidia wale wanaoonekana kupotea au tayari wmeshapotea kwa kuwaelemisha juu ya madhara ya vilevi na utumiaji wa madawa ya kulevya.

Kifo cha Albeart Mangwear ni fundisho kubwa kwa vijana na wanamuziki wa Tanzania juu ya athari za matumizi ya madawa ya kulevya, hivyo ni vyema kuhakikisha kwamba hatupotezi vipaji na nguvu mali zetu kwa mambo yanayozuilika.
 
Kuna haja ya Serikali na Tume ya Kuthibiti Madawa ya Kulevya kutilia mkazo suala hili ili jamii yetu isizidi kupotea, na sisi kama jamii kuhakikisha tunatoa ushirikiano kwa vyombo husika kuweza kufanikisha jitihada zinazofanywa nao ili tuweze kufanikisha malengo yake

Nina hakika hakuna ambaye hafahamu madhara yake ila ni vyema kukumbushana kwamba maisha bila vilevi inawezekana hata Muziki na Hip Hop Bila Madawa Inawezekana....
 

Copyright © 2009. MCHAMBUZI - Haki zote zimehifadhiwa